Na Mwandishi wetu
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imesema kuwa usafi wa mifereji ya majitaka iliyo nje ya mtandao (network) wa majitaka unaosimamiwa na mamlaka hiyo si jukumu lake, bali ni wajibu wa halmashauri husika.
Akijibu hoja iliyowasilishwa na Tafakari Media kuhusu mfereji wa majitaka unaopita eneo la Gardeni, Kinondoni, karibu na Bar ya Kiduli, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa DAWASA, Bi. Everlasting Lyaro, alisema DAWASA inahusika na usimamizi na usafi wa miundombinu ya mtandao wake wa majitaka pekee.
"Mifereji ya majitaka haiko DAWASA. Usafi wa mazingira unaosimamiwa na mamlaka ni wa network ya majitaka. Hizi nyingine ziko chini ya halmashauri husika," alifafanua Bi. Lyaro.
Hata hivyo, wananchi wengi bado wanaamini kuwa DAWASA ndiyo taasisi yenye jukumu la kwanza katika masuala yote yanayohusu majitaka na usafi wa mazingira, jambo linalosababisha sintofahamu pale changamoto kama hizi zinapotokea.
Mfereji huo unaopita karibu na bustani inayotumiwa na wananchi kupumzika umeelezwa kuwa unatoa harufu mbaya na kuzua hofu ya kuwepo kwa hatari ya kuenea kwa magonjwa ya mlipuko, ikiwemo kipindupindu na homa ya matumbo.
Kutokana na ufafanuzi huo wa DAWASA, sasa macho ya wananchi yanaelekezwa kwa Manispaa ya Kinondoni, ambayo imeelezwa kuwa ndiyo mamlaka yenye wajibu wa kushughulikia usafi wa mifereji hiyo na kuchukua hatua za kulinda afya na mazingira ya wananchi.






0 Comments