Na Mwandishi wetu
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), amekutana kwa mazungumzo na Balozi wa Finland nchini, Mhe. Theresa Zitting, katika kikao cha kumuaga kufuatia kukamilika kwa muda wake wa uwakilishi nchini Tanzania.
Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wamepongeza ushirikiano wa muda mrefu na wenye manufaa kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Finland, hususan katika sekta za misitu, madini, elimu, maendeleo, biashara na uwekezaji.
Aidha, pande zote mbili zimeeleza dhamira ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wa pande mbili pamoja na kushirikiana katika masuala ya kikanda na kimataifa yenye maslahi ya pamoja.
Mheshimiwa Kombo amemshukuru Balozi Theresa kwa mchango wake katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili, huku akimtakia kila la heri na mafanikio katika majukumu yake mapya.
Naye Balozi Theresa ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano alioupata katika kipindi chote cha uwakilishi wake nchini, akieleza kuwa ataendelea kuwa Balozi mwema wa ukarimu na rafiki wa Watanzania popote atakapokuwa.







0 Comments