Blog Post

TEKNOLOJIA YA M GAS RESOURCES YACHANGIA KUZUIA UHARIBIFU WA MISITU NCHINI




 Na Omary Mbaraka 

Teknolojia Kampuni ya M Gas Resources ambayo inasambaza majiko na gas ambayo mwananchi wa kima cha chini atamudu gharama zake imeweka mikakati mizito ili kuwafikia WANANCHI ambao hutumia mkaa kupikia jambo ambalo litapunguza kwa kiasi kikubwa ukataji wa misitu


Mkurugenzi wa Operesheni wa M-Gas Resources, Abdalah Kajangwa, amewahimiza Watanzania kuachana na matumizi ya mkaa na kuni kwa kuwa pia yana madhara makubwa kwa afya za binadamu na uchafuzi makubwa mazingira, badala yake watumie gesi ya kupikia inayosambazwa na kampuni hiyo.


Kajangwa ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kutoka Tafakari News Weblog,  Tafakari newspaper online na Global TV katika ofisi za M-Gas Resources. Katika ziara hiyo, waandishi walipata fursa ya kutembelea kitengo cha huduma kwa wateja, mafundi pamoja na kujionea namna kampuni hiyo inavyotoa huduma kwa kutumia teknolojia ya kisasa.


Amesema M-Gas Resources imeleta mfumo mpya unaowarahisishia wananchi kupata huduma ya gesi kwa kuwapatia jiko na mtungi kwa mkopo kupitia maafisa wa mauzo, ambapo mteja hulipa kiasi cha shilingi 750 kwa wiki hadi atakapomaliza deni lake.


Kwa mujibu wa Kajangwa, gharama hiyo ni nafuu ikilinganishwa na matumizi ya mkaa, ambapo familia nyingi hulazimika kutumia takribani shilingi 2,000 kununua kopo moja la mkaa. Amesema kwa kutumia gesi ya M-Gas, familia zinaweza kupika kwa gharama ndogo huku zikinufaika na huduma salama na ya kisasa.


Aidha, amekanusha dhana potofu kuwa gesi haiwezi kupika vyakula kama maharage au wali, akieleza kuwa matumizi sahihi ya jiko la gesi na mpangilio wa moto huwezesha kupika aina zote za vyakula kwa ufanisi.


Kajangwa amesema mitungi ya M-Gas imeunganishwa na teknolojia ya kisasa inayowezesha kampuni kufahamu mapema endapo gesi imekaribia kuisha au kunapotokea hitilafu, hatua inayosaidia kuongeza usalama na kuboresha huduma kwa wateja.


Katika hatua nyingine, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuondoa baadhi ya kodi kwenye vifaa vinavyotumika katika huduma za gesi, ikiwemo mita, akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza gharama za huduma na kuwafanya wananchi wengi zaidi kumudu matumizi ya gesi safi ya kupikia

Post a Comment

0 Comments

Close Menu