Na Moses Mwakibolwa
Magomeni, Kinondoni – Dar es Salaam
Wakazi wa Magomeni wameiomba Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuangalia kwa haraka hali ya usafi katika eneo la bustani maarufu kama Magomeni Gardeni, ambalo limekuwa sehemu muhimu ya mapumziko kwa wananchi, wazazi na watoto kwa muda mrefu.
Eneo hilo limekuwa likitumiwa na wakazi kupata upepo, hewa safi na sehemu ya kupumzika katikati ya shughuli za kila siku. Hata hivyo, wananchi wanasema hali ya sasa ya usafi imeanza kuleta changamoto kutokana na kuwepo kwa taka, mitaro ya maji na uchafu unaozunguka eneo hilo.
Baadhi ya wananchi wamesema kuwa ndani ya eneo hilo kuna miundombinu ya choo na bafu chini ya usimamizi wa DAWASA, lakini changamoto kubwa imekuwa ni usafi na utunzaji wa mazingira yanayolizunguka eneo hilo.
Mkazi wa maeneo ya Magomeni Gardeni, Aisha Athumani, amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakichangia tatizo kwa kutupa taka ovyo.
> “Eneo hili ni la wananchi wote, lakini baadhi ya watu wanatupa taka bila kujali. Inafika hatua mazingira yanakuwa machafu,” alisema.
Kwa upande wake, mfanyabiashara katika eneo hilo, Hamisi Juma, amesema wafanyabiashara wanaendelea kufanya shughuli zao lakini hakuna sehemu maalumu ya kutupia taka.
> “Tunafanya biashara hapa, lakini tunahitaji kuwepo na utaratibu mzuri wa taka ili eneo libaki safi,” amesema.
Wananchi pia wameeleza kuwa baadhi ya uchafu umeonekana karibu na mifereji ya maji ya DAWASA, hali ambayo wanaona inaweza kuathiri usafi wa mazingira na afya ya jamii.
Jitihada za kumpata Mwenyekiti wa Mtaa kwa ajili ya kupata maelezo zaidi hazikufanikiwa wakati wa kuandaa habari hii.
Wananchi wanaomba mamlaka husika, hususan DAWASA na viongozi wa eneo hilo, kufika katika bustani hiyo kufanya usafi, kuweka utaratibu wa ukusanyaji wa taka na kuhakikisha eneo hilo linaendelea kuwa kivutio salama kwa jamii.
DAWASA ina majukumu yanayohusisha huduma za maji na usafi wa mazingira, ikiwemo miundombinu ya usafi wa jamii.



0 Comments