Blog Post

WANAVIKUNDI WAMLILIA DKT SAMIA KWA MAAFISA MAENDFLEO KUJIKOPESHA

 Na Moses Mwakibolwa


Baadhi ya wanavikundi wameeleza malalamiko kuhusu utekelezaji wa mikopo ya asilimia 10 ya serikali kwa vikundi, wakidai kuwa baadhi ya walengwa wanakosa fursa ya kupata mikopo hiyo kutokana na changamoto za usimamizi katika ngazi za chini.


Wananchi hao wamesema kuwa badala ya baadhi ya vikundi kupewa elimu na kusaidiwa kuboresha vigezo ili waweze kunufaika katika awamu zinazofuata, kumekuwa na hali ya baadhi yao kunyimwa nafasi bila kupewa mwongozo wa kutosha.


Wamedai kuwa kuna baadhi ya watu wenye mishahara kutoka serikalini ambao wamekuwa wakijipatia mikopo hiyo, jambo ambalo wanaamini linakwenda kinyume na dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.


“Mikopo hii ililenga kuwafikia wananchi wenye uhitaji na kuwainua kiuchumi. Lakini kuna changamoto pale ambapo baadhi ya watu wanaotakiwa kusimamia mchakato wanakuwa wanufaika wenyewe au kuwasaidia watu wao wa karibu badala ya walengwa halisi,” alisema mkazi mmoja wa Magomeni ambaye hakutaka jina lake litajwe.


Aidha, wananchi wameomba kuwepo kwa uwazi zaidi katika utaratibu wa utoaji wa mikopo hiyo, ikiwemo kuweka wazi sifa za waombaji, namna ya kuchagua vikundi na kuhakikisha fedha zinawafikia walengwa.


Pia wametoa mfano wa mafunzo yanayotolewa na Vocational Education and Training Authority (VETA) kwa vijana, wakisema ni mpango mzuri wa kujenga uwezo, lakini ratiba na upatikanaji wake uzingatie mazingira ya vijana.


Wamesema vijana wanaotoka maeneo kama Mbweni au Bunju wanaweza kupata changamoto kusafiri hadi Temeke kwa ajili ya mafunzo bila ratiba rafiki, na wamependekeza baada ya mafunzo vijana hao pia wawezeshwe kupata mikopo au fursa za mitaji ili elimu hiyo iwe na matokeo.


Wananchi wameiomba serikali kuendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mikopo hiyo ili kuhakikisha malengo ya kuwawezesha wananchi kiuchumi yanatimia.

Post a Comment

0 Comments

Close Menu