Blog Post

MGOGORO WA KIWANJA CHA IBADA MBWENI KIKIUZWA


 Na Mwandishi wetu 

TAARIFA YA UCHUNGUZI: MGOGORO WA ENEO LA IBADA MBWENI NA TUHUMA ZA UUZAJI WA SEHEMU HIO YA KIWANJA

Taarifa kutoka kwa baadhi ya vyanzo vya ndani zinaeleza kuwa taasisi iliyo chini ya Kanisa Katoliki, Kolping Society of Tanzania, inadaiwa kuuza sehemu ya eneo la kiwanja lililopo jirani na Malindi Estate, Kata ya Mbweni, Manispaa ya Kinondoni, kwa wamiliki wa kiwanda cha uzalishaji wa video kilichopo pembezoni mwa eneo hilo.


Kwa mujibu wa taarifa hizo, eneo hilo lilinunuliwa na waumini wa Kanisa Katoliki kwa ajili ya ujenzi wa Parokia ya Yohane Mbatizaji, lakini hadi sasa waumini hao wanadai hawajapewa hati ya umiliki wa eneo hilo.


Waumini wanaoendesha ibada katika eneo hilo wameiomba Serikali Kuu kuingilia kati mgogoro huo ambao wameeleza kuwa umedumu kwa muda mrefu bila kupata suluhisho. Wanasema wanapata changamoto kufanya shughuli za ibada karibu na eneo linalodaiwa kuwa na kiwanda.


Baadhi ya waumini hao waliieleza Gazeti la TAFAKARI kuwa walinunua eneo hilo kutoka kwa watu waliodai kuwa wasimamizi wa eneo hilo kwa kiasi kinachozidi Shilingi milioni 150, lakini suala la umilikishaji wa hati bado halijakamilika.


Taarifa hizo zinaeleza kuwa Baraza la Wadhamini limekuwa likitafutwa ili kutoa ufafanuzi kuhusu suala hilo, lakini hadi sasa majibu rasmi hayajapatikana.


Wakati huohuo, wananchi wa maeneo jirani wameeleza kuwa kuna shughuli zinazofanyika katika jengo linalodaiwa kuwa kiwanda bila kuwa na bango au utambulisho wa wazi wa kampuni. Baadhi ya wakazi wanasema wamekuwa wakiona magari makubwa yakiingia usiku, jambo lililowafanya kuwa na hofu kuhusu aina ya shughuli zinazofanyika hapo.


Wananchi pia wamehoji kama mamlaka husika kama TRA, OSHA, NEMC na wakaguzi wa viwanda wamewahi kufanya ukaguzi wa eneo hilo.


Katika kikao cha mtaa, Mwenyekiti wa Mtaa huo, Selina Mkony, alipoulizwa kuhusu eneo hilo, alieleza kuwa wana taarifa kuwa eneo hilo lina vibali vinavyowawezesha kuendesha shughuli zao.


Hata hivyo, wananchi wanaendelea kuomba mamlaka husika kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini ukweli wa umiliki wa eneo, uhalali wa shughuli zinazofanyika na kuhakikisha usalama wa wananchi.


TAFAKARI inaendelea kufuatilia suala hili na itatoa taarifa zaidi baada ya kupata majibu kutoka kwa wahusika.

Post a Comment

0 Comments

Close Menu