Na Mwandishi wetu 


"RAIS DKT SAMIA AZITAKA BENKI KUJALI ZAIDI UAMINIFU BADALA YA KUWEKA VIKWAZO VYA DHAMANA KATIKA MIKOPO"

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza umuhimu wa kuwa na mipango ya mageuzi ya kiuchumi yenye lengo la kuhakikisha ukuaji wa uchumi hauishii kwenye takwimu bali unawanufaisha wananchi wa kawaida.


Amesema ni muhimu kwa taasisi za kiuchumi kuhakikisha zinatumia vyema sera na mipango iliyopo ili ukuaji wa pato la taifa (GDP) uweze kuonekana katika maisha ya kila siku ya wananchi.


“Kama tunavyoona kwingine, uchumi unapanda, GDP kubwa lakini ukifika kwa watu hali zao si nzuri, kwa hiyo tusiposimamia vyema mabadiliko haya yatabaki kuwa takwimu,” amesema Rais Samia.


Rais Samia ameyasema hayo Juni 12, 2026 katika maadhimisho ya miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.


Amesema ni muhimu kuhakikisha sekta zote za uchumi zinashirikiana ili maendeleo ya nchi yaweze kugusa wananchi moja kwa moja, badala ya kubaki katika ripoti na takwimu pekee.


"PIA RAIS DKT SAMIA AITAKA BOT KUHAKIKISHA GHARAMA ZA MIKOPO ZIWEKWE WAZI KWA WANANCHI"


Rais Samia Suluhu Hassan, ameielekeza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuweka mipango itakayosaidia taasisi zote za kifedha nchini kuongeza uwazi kuhusu gharama za mikopo inayotolewa kwa wananchi.


Amesema wananchi wanapaswa kupewa taarifa sahihi na kwa lugha rahisi kuhusu kiasi halisi watakacholipa pamoja na muda wa marejesho ya mikopo hiyo, hatua ambayo itasaidia kupunguza malalamiko yanayojitokeza kwa sasa.


Rais Samia ametoa maelekezo hayo, Juni 12, 2026, wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.


"PIA RAIS DKT SAMIA AMESEMA TUSIMNYIME MTU MKOPO KWA SABABU HANA MALI"


Rais Samia Suluhu Hassan, ameiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutafuta njia mbadala za kuwawezesha wananchi kupata mikopo hata kama hawana nyumba, magari au dhamana za kawaida zinazotumika na taasisi za kifedha.


Akizungumza jijini Dar es Salaam Juni 12, 2026 katika maadhimisho ya miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania, Rais Samia amesema wananchi wenye biashara, historia nzuri ya mauzo na kumbukumbu za miamala wanapaswa kupewa nafasi ya kupata mikopo.


Amesisitiza kuwa taasisi za fedha zinapaswa kutambua uaminifu wa mteja kama kigezo muhimu katika utoaji wa mikopo.


“Tusimnyime mtu mkopo kwa sababu hana mali tulizozizoea wakati ana historia inayoonesha wazi kuwa anaaminika. Uaminifu ni mali kubwa kuliko hata mali inayoonekana,” amesema Rais Samia.

Hata hivyo hivi karibuni Waziri wa habari Mhe Paul Makonda alitoa fungu kubwa kwa ajili ya kuwakopesha watengeneza maudhui (Content Creators)  Lakini Mwandishi wa Habari hizi alipofika BENKI ya CRDB tawi la mlimani aliambiwa atapaswa kutoa dhamana ya nusu ya mkopo na nusu nyingine ni dhamana ya Baraza la Sanaa jambo ambalo wengi watengeneza maudhui watakwama na lengo la waziri huyo wa habari halitafanikiwa ipasavyo