Blog Post

BRELA YALALAMIKIWA NA WANANCHI KATIKA MAOMYESHO YA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA DAR ES SALAAM

 Na Moses


Katika Maonesho ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma jijini Dar es Salaam mwaka 2026, baadhi ya wananchi wameeleza kutoridhishwa na huduma wanazodai kupokea kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), huku wengine wakimfuata Mkurugenzi wa taasisi hiyo kuwasilisha malalamiko yao.


Mwananchi Nurdin Ramadhani amesema alifika kwenye maonesho hayo kwa lengo la kupata huduma lakini hakuridhishwa na namna suala lake lilivyoshughulikiwa.


Amesema kuna changamoto kuhusu kampuni yake, ambapo anadai kulikuwa na jaribio la kumuondoa katika kampuni hiyo kinyume na taratibu.


"Nimewasilisha malalamiko kuhusu nyaraka zangu ambazo zimefichwa na kugushiwa ili mimi niondolewe kwenye kampuni. Sijasaini karatasi yoyote wala kuandika barua ya kuondoka kwenye kampuni wakati mimi ni mwanahisa," amesema Nurdin Ramadhani.


Kwa upande wake, Aisha Ramadan amehoji namna mabadiliko ya taarifa za umiliki wa kampuni yanavyoweza kutokea wakati bado mifumo mingine ya Serikali ikimtambua kama mhusika.


"Kwa nini TRA kwenye mfumo wao mpaka leo bado wananitambua na kunihudumia vizuri kwenye masuala ya kodi? Kwa nini mifumo isiingiliane pale unapofanya usajili? TRA wapo kuwahudumia wafanyabiashara kwenye kodi, lakini BRELA pia ni sehemu muhimu ya taarifa za biashara. Kukosekana kwa muunganiko wa taarifa kunaleta usumbufu mkubwa kwa wananchi," amesema.


Wananchi hao wameiomba Serikali kufanya uchunguzi ili kubaini kama kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu na kuhakikisha haki za wamiliki wa kampuni zinalindwa.


Aidha, wameitaka BRELA kuongeza elimu kwa wafanyabiashara kuhusu taratibu za usajili, mabadiliko ya umiliki na ulinzi wa taarifa za kampuni, ili kuzuia mianya ya watu kutumia nyaraka za kughushi kuanzisha au kubadilisha taarifa za kampuni bila ridhaa ya wahusika.


"Kama hakuna elimu ya kutosha kuhusu taratibu za biashara, ni vigumu kuwasaidia wafanyabiashara. Mtu anaweza kughushi nyaraka, kutumia watu wengine na kuendesha mchakato wa kampuni bila mwenye kampuni kujua. Tunataka kujua kwa nini hatua kali hazichukuliwi pale ukiukwaji kama huu unapojitokeza," wameeleza wananchi hao.


Wananchi wameomba mifumo ya taasisi za Serikali zinazohusika na biashara kuimarishwa ili taarifa za wafanyabiashara zilindwe na migogoro ya aina hiyo ipungue.

Post a Comment

0 Comments

Close Menu