Blog Post

WANANCHI WA MALINDI ESTATE WATISHIA KUIPELEKA SERIKALI MAHAKAMANI





 Na Mwandishi wetu 


Maelfu ya wananchi wa Mtaa wa Malindi Estate, Wilaya ya Kinondoni, wameazimia kuiburuza mahakamani Serikali kwa madai ya kugawa maeneo ya umma kwa watu binafsi bila kufuata taratibu za kisheria.


Hatua hiyo imekuja kufuatia malalamiko ya wananchi kuhusu uwepo wa maafisa wanaodaiwa kufika eneo hilo kwa ajili ya upimaji wa viwanja bila kutoa utambulisho rasmi unaoeleza mamlaka au sababu za shughuli hizo.


Akizungumza Mtendaji wa Mtaa wa Malindi, Kakaa Bonamax, alidai kuwa maafisa hao walifika bila kuwa na nyaraka za utambulisho kutoka kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, hali iliyozua taharuki na maswali mengi miongoni mwa wakazi wa eneo hilo. Iweje maafisa waje bila utambulisho?


“Eneo hili lilishapimwa na kugawiwa wananchi kwa mujibu wa taratibu zilizokuwepo. Sasa tunaona watu wanakuja tena kupima bila maelezo ya kutosha. Wananchi wanahitaji ufafanuzi wa moja kwa moja kutoka kwa Mkurugenzi ili kuondoa sintofahamu iliyopo,” alisema.


Wananchi hao wameiomba Manispaa ya Kinondoni kutuma viongozi wake wakuu kufika eneo hilo na kuzungumza nao moja kwa moja badala ya kuendelea kutuma maafisa ambao hawatoi maelezo yanayoridhisha.


Katika mkutano wa wananchi uliofanyika wiki iliyopita, ilielezwa kuwa baadhi ya maeneo yaliyokuwa yametengwa kwa matumizi ya umma, ikiwemo shule, soko, kituo cha daladala na taasisi za kifedha, yameanza kupimwa kwa lengo la kugawiwa watu binafsi wanaodaiwa kuwa na ushawishi mkubwa serikalini.


Wananchi walieleza wasiwasi wao kuwa iwapo maeneo hayo yatabadilishwa matumizi, jamii itakosa huduma muhimu ambazo zilitarajiwa kupatikana katika eneo hilo kadiri idadi ya wakazi inavyoendelea kuongezeka.


Kutokana na hali hiyo, wananchi wameunda kamati maalum ya watu tisa yenye jukumu la kufuatilia nyaraka, taratibu za upangaji na ugawaji wa ardhi pamoja na kufanya uchunguzi wa kina kuhusu hatua zinazochukuliwa na maofisa ardhi wa Wilaya ya Kinondoni.


Walisema kamati hiyo pia itashirikiana na wataalamu wa sheria ili kubaini kama kuna ukiukwaji wa sheria za ardhi na mipango miji, kabla ya kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika.


Wananchi hao wameitaka Serikali kuingilia kati haraka ili kuzuia migogoro ya ardhi inayoweza kujitokeza na kuhakikisha maeneo yaliyotengwa kwa manufaa ya umma yanabaki kutumika kwa maslahi ya wananchi wote.


Hata hivyo, juhudi za kupata maelezo kutoka kwa viongozi wa Manispaa ya Kinondoni kuhusu madai hayo hazikufanikiwa mara moja hadi taarifa hii inaandaliwa.

Post a Comment

0 Comments

Close Menu