*NAIBU WAZIRI AYOUB AHIMIZA MAGARI KUINGIA KWENYE MFUMO WA VIMIS*
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Ayoub Mohammed Mahmoud, amewataka wamiliki wa magari nchini kuyaingiza kwenye Mfumo wa Vehicle Inspection Management Information System (VIMIS) na kukamilisha ukaguzi wake ifikapo Julai 31 mwaka huu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam baada ya kupokea taarifa ya tathmini ya utendaji wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Mahmoud amesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha usalama barabarani na kupunguza ajali nchini.
Kwa upande wake, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, SACP William Mkonda, amesema hadi sasa magari 400 yamekaguliwa kupitia VIMIS.
Aidha, imeelezwa kuwa mfumo huo wa VIMIS umeanzishwa ili kurahisisha usajili na ukaguzi wa magari, pamoja na kuhakikisha vyombo vyote vya moto vinavyotumika nchini vinakidhi viwango vinavyotakiwa vya usalama.
VIMIS ni mfumo wa kidijitali unaotumika kusimamia usajili, ratiba, ufuatiliaji na kumbukumbu za ukaguzi wa magari nchini. Mfumo huu unalenga kuhakikisha magari yanayoruhusiwa kutumika barabarani yanakidhi viwango vya usalama na ubora vinavyotakiwa, hivyo kusaidia kupunguza ajali zinazotokana na hitilafu za kiufundi pamoja na kuongeza ufanisi na uwazi katika huduma za ukaguzi wa magari.



0 Comments