Blog Post

MHE KOMBO WAZIRI WA MAMBO YA NJE AZUNGUMZA NA WAFANYABIASHARA WAKUBWA WA KOREA


 Na Mwandishi wetu 


Jumuiya ya wafanyabiashara wakubwa wa Jamhuri ya Korea imethibitisha nia yake ya kuendelea kushirikiana na Tanzania katika uwekezaji na biashara, huku ikipongeza hatua kubwa zilizofikiwa katika kuimarisha sekta za miundombinu nchini, ikiwemo barabara, reli, bandari na huduma za usafirishaji. 


Hayo yameelezwa tarehe 31 Mei 2026 jijini Seoul, wakati wa mazungumzo kuhusu fursa za uwekezaji na biashara kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea yaliyofanyika kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo na viongozi wa jumuiya hiyo. 


Wqkati wa mazungumzo hayo, yaliyoambatana na chakula cha mchana cha kikazi, wafanyabiashara hao walipongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuimarisha miundombinu inayorahisisha biashara na uwekezaji nchini. 


Wametaja miradi mikubwa ya kimkakati, hususan Reli ya Kisasa (SGR) na maboresho ya huduma za bandari na usafirishaji, kuwa miongoni mwa vivutio vikuu vinavyowahamasisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Jamhuri ya Korea kuangalia kwa karibu zaidi fursa zilizopo Tanzania. 


Kwa upande wake, Mhe. Balozi Dkt. Kombo aliishukuru jumuiya hiyo ambayo baadhi ya wanachama wake tayari wanawekeza nchini, kwa kuonesha dhamira ya dhati ya kuendelea kuwekeza Tanzania. Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara ili kuvutia mitaji zaidi ya kigeni, na kuwakaribisha wawekezaji wa Korea kuja kwa wingi kuwekeza katika sekta mbalimbali za maendeleo. 


Jumuiya hiyo ilijumuisha wafanyabiashara wanaomiliki na kuongoza kampuni kubwa za Korea zinazojihusisha na ujenzi, ukandarasi wa kimataifa na biashara ya uagizaji wa bidhaa. Miongoni mwa taasisi zilizoshiriki ni Chama cha Waagizaji Bidhaa cha Korea (KOIMA) na Chama cha Wakandarasi wa Kimataifa cha Korea (ICAK). 


Mhe. Balozi Dkt. Kombo yuko nchini Korea kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika na Korea unaofanyika kuanzia tarehe 31 Mei hadi 2 Juni 2026.

Post a Comment

0 Comments

Close Menu