Na Mwandishi wetu
Mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati, hususan vita inayohusisha Iran, umeanza kuleta mtikisiko mkubwa katika sekta ya mbolea duniani na kuzua hofu ya kuporomoka kwa uzalishaji wa chakula ikiwa hali hiyo itaendelea kwa muda mrefu.
Tofauti na mishtuko ya awali iliyosababishwa na janga la UVIKO-19 na vita ya Urusi na Ukraine, mgogoro huu mpya umeibuka wakati ambapo masoko ya kimataifa na minyororo ya usambazaji bado iko katika hali ya kupona, jambo linaloongeza uzito wa athari zake.
Changamoto kubwa inayojitokeza sasa ni uwezekano wa kuvurugika kwa muda mrefu kwa usambazaji wa mbolea duniani, hali ambayo inaweza kuhatarisha moja kwa moja uzalishaji wa kilimo na usalama wa chakula kwa mamilioni ya watu.
Chanzo kikuu cha mshtuko huu ni vikwazo vya usafirishaji katika Mlango wa Hormuz njia nyeti ya baharini inayounganisha Ghuba ya Uajemi na masoko ya dunia.
Eneo hilo lina umuhimu mkubwa kimkakati kwani mwaka 2024 lilipitisha hadi asilimia 30 ya biashara ya mbolea duniani, pamoja na takribani asilimia 20 ya gesi asilia iliyosafirishwa kimataifa na asilimia 27 ya mafuta ya biashara ya dunia.
Hatua ya Iran kupunguza au kudhibiti usafirishaji katika njia hiyo, ikiwa ni sehemu ya majibu yake dhidi ya mashambulizi ya Marekani na Israel, tayari imesababisha kupanda kwa bei za nishati na mbolea katika masoko ya dunia.
Zaidi ya hayo, mashambulizi ya pande zote mbili yameharibu miundombinu muhimu ya uzalishaji na usafirishaji, ikiwemo vituo vya gesi kama Ras Laffan Industrial City nchini Qatar na kituo kikubwa cha mafuta cha Kharg Island nchini Iran.
Endapo mashambulizi yataendelea, upungufu wa bidhaa hizo unaweza kuwa mkubwa zaidi.
UMUHIMU WA GHUBA KATIKA UZALISHAJI WA MBOLEA
Kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita (2023–2025), nchi za Ghuba zimekuwa kitovu kikuu cha uzalishaji na usambazaji wa mbolea duniani.
Eneo hilo limeongoza kwa usafirishaji wa mbolea za nitrogeni (urea na ammonia) na kushika nafasi ya pili kwa mbolea za fosfeti kama DAP na MAP.
Pia, gesi asilia inayotoka katika eneo hilo ni muhimu kwa nchi nyingi zinazozalisha mbolea lakini hazina vyanzo vya ndani vya nishati, zikiwemo India, Pakistan, Bangladesh na Türkiye



0 Comments