Na Omary Mbaraka
Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) imepanga kujenga kituo cha mfano cha kuchenjua madini ya dhahabu kwa kutumia teknolojia ya kisasa katika eneo la Mwakitolyo katika mwaka wa fedha 2026/27, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha wachimbaji wadogo kuongeza tija na thamani ya madini yao.
Kauli hiyo imetolewa leo Mei 07, 2026 Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Mwanahamisi Athuman.
Dkt. Kiruswa amesema ujenzi wa kituo hicho ni sehemu ya mkakati wa Serikali kupitia STAMICO wa kuwaendeleza na kuwaimarisha wachimbaji wadogo nchini. Ameeleza kuwa vituo vingine vya mfano vimejengwa katika mikoa ya Geita na Mara Mbeya.
Aidha, amesema mkandarasi wa utekelezaji wa mradi wa kituo cha Mwakitolyo tayari amepatikana na kwamba hatua za mwisho za kimkakati zikikamilika, ujenzi utaanza rasmi.
“Usanifu wa kituo hicho tayari umekamilika na kitakuwa na uwezo wa kuchenjua tani 120 za mbale kwa siku,” amesema Dkt. Kiruswa.
Ujenzi wa kituo hicho unatarajiwa kuongeza ufanisi katika shughuli za uchimbaji mdogo, kukuza ajira pamoja na kuongeza mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa Taifa.



0 Comments