*HOTUBA KUNTU YA MHE. WAZIRI WA AFYA ILIYOJIKITA KATIKA KUIBUA NA KUKUZA, KUILINDA TIBA ASILI KATIKA MIFUMO YA KISHERIA NA KIDIGITALI - INDIA.*
TANZANIA inaendelea kubadilisha TIBA ASILI kutoka katika hekima ya kurithiwa kizazi hadi kizazi, na kuifanya kuwa tiba inayothibitishwa KISAYANSI, inalindwa kidijitali, na yenye uwezo wa kibiashara kwa manufaa ya afya duniani kote.
*TIBA ASILI KULINDWA KISHERIA*
TUNAAMINI kuwa tiba asilia, inapolindwa na SHERIA, ikiimarishwa na SAYANSI, ikiwezeshwa na TEKNOLOJIA, na kuendeshwa kwa mtazamo wa KIBIASHARA, inaweza kuwa nguzo muhimu ya kimataifa katika kujenga jamii zenye AFYA BORA.
TUPO hapa India tukiwa tayari KUJIFUNZA, tayari KUONGOZA, na tayari KUSHIRIKIANA.
TIBA asilia bado ni muhimili muhimu wa HUDUMA ZA AFYA ya msingi nchini Tanzania, ambapo takribani asilimia 60 ya wananchi wetu hutumia huduma za waganga wa tiba asilia, ama kabla au sambamba na huduma za hospitali za kisasa.
UHALISIA huu unaonesha kuwa upatikanaji wa ushahidi wa kisayansi si hiari bali ni jambo la lazima.
*USALAMA NA UBORA WA TIBA ASILI NA TAFITI.*
TUNAUNGA mkono kikamilifu Mkakati wa Kimataifa wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wa Tiba Asilia wa mwaka 2025–2034, hususan katika eneo la kujenga ushahidi wa USALAMA, UFANISI na UBORA wa tiba asilia.
TUNATOA kipaumbele kwa TAFITI za gharama nafuu zinazofanywa katika jamii, kwa kushirikiana na taasisi zetu za utafiti, MAABARA na VYUO VIKUU.
INGAWA tunakaribisha ushirikiano katika TAFITI, uthibitisho na ujenzi wa uwezo, ni muhimu kutambua kuwa ushahidi unaweza kuwalinda wagonjwa pale tu unapoungwa mkono na mifumo imara ya udhibiti na uhakiki wa ubora.
*SHERIA ZA TANZANIA NA TIBA ASILI.*
TANZANIA imeweka msingi thabiti wa kisheria na kikanuni kupitia Sheria ya TIBA ASILI na Tiba Mbadala Na. 23 ya mwaka 2002, inayotekelezwa na BARAZA LA TIBA ASILI NA TIBA MBADALA.
*TAASISI ZETU NA TIBA ASILI.*
TUNAENDELEA kuimarisha taasisi zinazohusika na tathmini ya USALAMA na UBORA, zikiwemo TMDA, GCLA, NIMR na taasisi nyingine husika. Lengo letu ni kuifanya tiba asilia iwe ya KITAALAMU huku tukiilinganisha na viwango vya kimataifa vya ubora na USALAMA.
*TIBA ASILI NA MFUMO RASMI, BIMA YA AFYA KWA WOTE*
HATUA inayofuata ni kuunganisha tiba asilia katika MFUMO RASMI wa huduma za afya. Tanzania imejizatiti kuingiza tiba asilia katika huduma za afya ya msingi ili kuunga mkono lengo la BIMA YA AFYA KWA WOTE tangu mwaka 2023.
HUDUMA za tiba asilia tayari zimeanza kutolewa katika hospitali rasmi, ambapo BIDHAA 27 ZA TIBA ASILI zilizothibitishwa zinatumika katika matibabu ya magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza.
*MKAKATI WA KUANZISHWA MITAALA YA TIBA ASILI.*
MKAKATI wetu unajumuisha kuanzisha MITAALA ya kitaifa ya TIBA ASILI, kutoa mafunzo kwa madaktari wa tiba ya kisasa na wataalamu wa tiba asilia, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya WAGANGA WA JADI na watoa huduma za afya ya KISASA.
MARA baada ya kuunganishwa katika utoaji wa huduma za afya, tiba asilia pia inakuwa chachu muhimu ya UBUNIFU na UKUAJI wa uchumi.
*HATUA ILIYOFIKIWA BIDHAA TIBA ASILI.*
HADI sasa, BIDHAA 141 za TIBA ASILI ZIMESAJILIWA nchini Tanzania, ambapo zaidi ya asilimia 90 huzalishwa na wajasiriamali wadogo wa ndani, kwa kuongozwa na Mpango Mkakati wa Sekta ya Afya.
*UCHUMI NA MIMEA TIBA*
Tanzania inakuza ushirikiano kati ya sekta ya UMMA na BINAFSI ili kuimarisha kilimo cha MIMEA TIBA, uchakataji na utengenezaji wa dawa, ubora wa uzalishaji, upatikanaji wa MASOKO na mauzo ya NJE.
TUNAKARIBISHA ushirikiano katika TEKNOLOJIA, uhamishaji wa teknolojia na UBUNIFU ili kuhakikisha bidhaa za tiba asilia za TANZANIA 🇹🇿 zinakidhi viwango vya masoko ya kimataifa.
*SUALA LA HAKI, MAADILI NA MAARIFA KUHIFADHIWA*
HATA hivyo, biashara ya tiba asilia lazima iwe ya KIMAADILI, JUMUISHI, na ilinde jamii ZILIZOHIFADHI MAARIFA haya kwa vizazi vingi. Kwa sasa, sehemu kubwa ya maarifa ya tiba asilia nchini Tanzania bado hayajaandikwa wala kulindwa kisheria. Ndiyo maana tunaendelea KUANDAA MIFUMO YA KISHERIA na KIMAADILI ya HAKI MILIKI ili kulinda maarifa ya asili na kuhakikisha mgawanyo wa faida kwa HAKI.
AHSANTENI SANA.
*Mhe. Mohamed O Mchengwerwa. (MMK)*
*Waziri wa Afta Tanzania 🇹🇿*



0 Comments