Na Mwandishi wetu 


Mbunge wa Jimbo la Makunduchi, na naibu waziri wa elimu na sayansi Mhe. Wanu Hafidh Ameir amewashukuru wakaazi wa Shehia ya Mtende kwa kumchagua na kumpa ridhaa ya kuwaongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo (2025-2030).


Mhe. Wanu ametoa shukrani hizo mnamo Desemba 25, 2025 wakati wa ziara yake ya Jimbo la Makunduchi katika Shehia ya Mtende na kusema ushiriki wao mkubwa katika kupiga kura umefanya wagombea wa ngazi zote kuibuka na ushindi wa kishindo.


Mhe. Wanu ameendelea kutoa shukurani za dhati na kuongeza kuwa Wanamtende hawajafanya makosa kwani wamechagua viongozi ambao ni turufu kubwa na kuaminiwa na Serikali katika ngazi za juu za Serikali ya Muungano pamoja na Zanzibar, ambapo Mhe. Wanu ni Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Mbali na kutoa shukrani hizo, Mhe. Wanu amepokea maoni na changamoto mbalimbali kutoka kwa wakaazi wa Shehia ya Mtende.


Changamoto moja wapo iliyoibuliwa ni kuhusu kukosekana kwa uhakika wa gari maalumu ya kusafirisha wagonjwa 'Ambulance', ambapo Mhe. Wanu ameahidi kutoa fedha kwaajili ya mafuta ili kurahisha usafirishaji wa wagonjwa pale inapohitajika.


Kuhusu kukosekana kwa mtambo wa Ultrasound, Mhe. Wanu amesema atawasilisha kwa Serikali na kulisimamia kikamilifu, huku akiahidi kuboresha maabara ya Skuli kwa kutoa vifaa ili kurahisha mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi.


Kadhalika, Mhe. Wanu amesema atawezesha SACCOS ya Kizimkazi kwaajili ya kuwezesha wajasiriamali kupata mikopo nafuu isiyo na riba ili kuwakwamua kiuchumi.


Aidha, Mhe. Wanu ameahidi kusaidia kufanya marekebisho madogo kwenye uwanja wa mpira wa Mtende na kuongeza kuwa atashirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine kupata ufadhili ili kujenga Akademi ya Michezo kwaajili ya kusaidia kuibua vipaji vya vijana mbalimbali.


Vile vile, Mhe. Wanu amekemea vitendo vya wanafunzi kujihusisha na shughuli za utalii na kuwahimiza kusoma ili kutengeneza mazingira mazuri ya maisha yao ya baadaye.