Na Mwandishi wetu 


OWM-TAMISEMI, Dar es salaam


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali inakusudia kufanya maboresho ya maeneo yote ya masoko nchini ili kuwawezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa amani nyakati zote za masika na kiangazi.


Dkt. Nchemba ameyasema hayo jana Desemba 29, 2025, alipokuwa akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara mara baada ya kukagua utekelezaji wa mradi wa Soko la Machinga Bunju B pamoja na miradi inayoendana na ujenzi wa soko hilo, ikiwemo ujenzi wa kituo cha mabasi madogo (stendi) na ukarabati wa barabara ya kuingia katika stendi hiyo iliyopo Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.


Amesema baadhi ya masoko bado yanakabiliwa na changamoto ya kujaa maji wakati wa msimu wa masika, hali inayosababisha kudorora kwa shughuli za kibiashara pindi mvua zinaponyesha. Ameeleza kuwa Serikali inalenga kuhakikisha Watanzania wanafanya biashara katika mazingira rafiki, salama na yenye kuvutia kwa wafanyabiashara na wateja wao.


Ili kufanikisha hilo, Dkt. Nchemba amewaagiza viongozi wa ngazi zote kuwafikia wafanyabiashara katika maeneo ya masoko ili kusikiliza kero zao na kufanya tathmini itakayoiwezesha Serikali kutatua changamoto hizo kwa wakati.


“Na huu ni wito wangu kwa viongozi wote, hasa maafisa biashara; nendeni waliko wananchi, fikeni wanakofanyia kazi, jueni wana kero gani. Suluhisho siyo kuwanyang’anya mabango wakati wa ziara za viongozi, bali ni kutatua kero zao,” amesema Dkt. Nchemba.


Kadhalika, Mhe. Nchemba ameahidi kuwasiliana na Wizara ya Fedha ili kutafuta kiasi cha Shilingi Bilioni 2.3 kinachohitajika kukamilisha ujenzi wa miradi yote mitatu katika eneo la Bunju B, ili iweze kukamilisha na kuanza kutoa huduma kwa wananchi mapema mwezi Machi 2026.


Awali, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Jafar Seif, amemhakikishia Waziri Mkuu kuwa TAMISEMI itaendelea kutekeleza miradi yote ya kipaumbele na kimkakati kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali.