Blog Post

MBUNGE MARIAM MUNGULA AONGOZA WABUNGE WA TANZANIA KUSHIRIKI KIKAO CHA KWANZA CHA BUNGE LA SABA LA AFRIKA(PAP)

Na Mwandishi wetu 


Ujumbe wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ukiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Mariam Mungula (Mb), umeshiriki ufunguzi rasmi wa Kikao cha Kwanza cha Bunge la Saba la Afrika (PAP), kinachofanyika Mjini Midrand, nchini Afrika Kusini.


Kikao hicho kilifunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Cyril Ramaphosa, ambaye katika hotuba yake alisisitiza umuhimu wa mshikamano na ushirikiano miongoni mwa nchi za Afrika katika kuimarisha demokrasia, kudumisha amani, kuharakisha maendeleo endelevu na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.


Katika hafla hiyo, Rais wa Bunge la Afrika (PAP), Mhe. Fateh Boutbig, aliwasilisha Dira ya Bunge hilo inayolenga kuimarisha mageuzi ya taasisi, kuongeza ufanisi wa utendaji, kuimarisha ushirikiano kati ya nchi wanachama, na kuhakikisha shughuli za Bunge hilo zinatoa matokeo yenye manufaa kwa wananchi wa Bara la Afrika.


Ushiriki wa Tanzania katika kikao hicho unaendelea kudhihirisha dhamira yake ya kuimarisha ushirikiano wa mabunge barani Afrika na kuchangia mijadala pamoja na maamuzi yanayolenga kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi, kuimarisha utawala bora, kudumisha amani na usalama, pamoja na kuendeleza utekelezaji wa Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika.


Post a Comment

0 Comments

Close Menu