*TANZANIA YAIMARISHA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA HURIA KUJENGA UHURU WA KIDIJITALI.*
Na Mwandishi Wetu, WMTH - New York, Marekani.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Kairuki (Mb), amesema Tanzania inaendelea kutumia Teknolojia Huria (Open Source) kama nyenzo muhimu ya kuharakisha mageuzi ya kidijitali katika utoaji wa huduma za umma, kujenga uhuru wa kidijitali na kuimarisha mifumo inayokidhi mahitaji ya wananchi.
Waziri Kairuki ameyasema hayo Juni 25, 2026 akihutubia katika Wiki ya Kimataifa ya Maadhimisho ya Teknolojia Huria (UN Open Source Week 2026) iliyofanyika Mjini New York, Marekani.
Amesema hatua hiyo inawezesha Serikali kumiliki na kudhibiti kikamilifu miundombinu yake ya kidijitali pamoja na kulinda taarifa muhimu za Serikali.
Aidha, ameeleza kuwa Tanzania imeweka mazingira wezeshi kupitia sheria na mifumo mbalimbali ikiwemo Sheria ya Mamlaka ya Serikali Mtandao ya mwaka 2020, na Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (Sura ya 44) ya mwaka 2023 hali iliyowezesha nchi kuwa na miongozo na utaratibu mahususi wa ujenzi wa mifumo ya kidijitali kwa taasisi za umma kwa kutumia teknolojia huria.
Ameongeza kuwa, mifumo mingi ya Serikali imejengwa kwa kutumia teknolojia hizo, hatua inayopunguza gharama za leseni za programu na kuongeza ufanisi wa huduma.
Amesema Serikali imeimarisha usimamizi wa mifumo ya kidijitali kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), ambayo ina jukumu la kuweka viwango na kuhakikisha taasisi za umma zinazingatia miongozo ya kiufundi. Hatua hiyo imechangia kuimarisha usalama wa taarifa, ushirikiano wa mifumo, kutumia wataalamu wa ndani kufanya ujenzi na kusimamia mifumo na hivyo kuweka matumizi bora ya rasilimali za Serikali.
Vilevile, Waziri Kairuki ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuwekeza katika kuwajengea uwezo watumishi wa umma ambapo zaidi ya watumishi 500 wamepatiwa mafunzo ya Teknolojia Zinazoibukia ili kuongeza uwezo wa ndani wa kubuni na kuendeleza mifumo ya Serikali.
Waziri Kairuki amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya viongozi, wabunifu wa teknolojia na wadau mbalimbali ni muhimu katika kujenga taifa lenye uhuru wa kidijitali na maendeleo endelevu yanayowanufaisha wananchi wote.
https://www.instagram.com/p/DaD6rcmCDnq/?igsh=NnR3MTk5bjJuN2V4



0 Comments