Na Steven Mhando
Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wassira, amewashushia rungu viongozi wa CHADEMA wanaobeza umri wake, akisisitiza kuwa uongozi haupimwi kwa miaka bali kwa uwezo wa kufikiri na maono thabiti.
Akizungumza leo Januari 29, 2025, katika mkutano wa hadhara mkoani Geita, Wassira aliwakemea Tundu Lissu na John Heche, akiwataka waache propaganda zisizo na mashiko.
“Mimi nina umri mkubwa lakini akili ni za miaka 55. Heche akitaka aende akaulize madaktari wa India na Muhimbili, watamwambia nina akili timamu kabisa. Gari ni injini, siyo bodi,” alieleza.
Akiwazungumzia Lissu na Heche, Wasira aliwakosoa kwa kushabikia ajenda za kigeni zisizoendana na misingi ya taifa.
“Waende Marekani wakaulize kwa nini Trump alichaguliwa tena badala ya Kamala Harris kama umri ndio hoja yao. Kwa sababu yeye na wale wanaooana wanaume kwa wanaume na wanawake kwa wanawake wapo huko Amerika, awafuate wenzake wamueleze sababu,” alisema kwa msisitizo.
Kwa kauli zake zenye uzito, Wassira amesisitiza kuwa uzoefu wake wa muda mrefu katika siasa ni mtaji wa kuwahudumia wananchi kwa ufanisi, huku akiwataka CHADEMA kuacha hoja nyepesi zisizo na mashiko.
0 Comments