Blog Post

DKT MWIGULU AAGIZA WANANCHI MUFINDI WALIPWE

 Na Mwandishi wetu 


_Ni za madai ya zaidi ya miaka mitatu iliyopita_


WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amefanikisha kulipwa papo hapo madeni ya wananchi wa Mufindi yenye thamani ya sh. milioni 5.6 kutokana kazi walizofanya kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi.


Madeni hayo ni ya kikundi cha vijana cha Ibantu ambao walikuwa wanadai sh. milioni 3.9 na fundi ujenzi wa vyoo ambaye alikuwa anadai sh. milioni 1.5 tangu mwaka 2022. Kikundi cha Ibantu kilipewa tenda ya kufyatua matofali 15,600 ambayo waliikamilisha.


Hayo yamejiri leo (Jumamosi, Mei 2, 2026) wakati Waziri Mkuu akisikiliza kero za wananchi wa Igowole, wilayani Mufindi, mkoani Iringa katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa shule ya msingi Igowelo ambako pia alisikiliza kero za wananchi.


Mmoja wa vijana wa kikundi hicho, Steven Adrian alisema: “Tulikamilisha kazi ya kufyatua matofali 15,600 tangu mwaka 2022 na kwa mujibu wa mkataba kila tofali lilikuwa ni sh. 250 lakini hadi sasa hatujalipwa hela yoyote. Sisi kwa unyonge wetu, tunabaki tunaugulia ndani kwa ndani. Hivyo tunaomba Waziri Mkuu utusaidie.” 


Alipoulizwa kama waliyapokea matofali hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Mashaka Mfaume alikiri kuwa matofali hayo yalipokelewa na Mhandisi wa Wilaya na yakatumika. 


Mkazi mwingine aliyenufaika na ziara ya Waziri Mkuu ni Christopher Mwangoka ambaye alipewa kazi na Halmashauri hiyohiyo ya kujenga matundu 10 ya vyoo na kichomea taka kwa gharama ya sh. milioni 6 lakini akalipwa sh. milioni 4.5 na akabakia anadai sh. milioni 1.5 tangu mwaka 2022.


Alipoulizwa kuwa watamlipa lini, Mkurugenzi alisema wako tayari kumlipa ndipo Waziri Mkuu akaagiza yeye, Mkuu wa Wilaya hiyo, Dkt. Linda Salekwa wakae na maafisa wao wajichangishe na kuwalipa wahusika hao kabla hajamaliza mkutano wake. Na wakati akihitimisha mkutano huo, alithibisha kuwa watu hao wamelipwa fedha zao.


Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa maagizo ya kuanza mara moja kwa utekelezaji wa miradi ya barabara za Nyololo – Igowole - Mtwango na ile ya Mafinga hadi Mgololo ili maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yatekelezwe kwa haraka.


Dkt. Mwigulu amemwelekeza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Iringa ahakikishe mkandarasi anapatikana ndani ya wiki mbili na wampatie majibu kuwa kazi hiyo imeshakamilika. “Mkuu wa Mkoa wewe ni Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara, kwa hiyo simamia suala hilo. Ndani ya wiki mbili mkandarasi apatikane, ahadi ya Mheshimiwa Rais ianze kutekelezwa,” amesema.


Kuhusu barabara ya Mafinga hadi Mgololo, Waziri Mkuu amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Doris Kalasa aandike barua hiyo leo hii kwenda Wizara ya Fedha kwa wakiomba wapatiwe fedha za malipo ya awali (advance payment) za mradi huo.


“Andikeni barua leo leo, ipelekeni Wizara ya Fedha kwa ajili ya kupatiwa fedha, na nakala nileteeni ofisini kwangu Jumatatu niione. Mradi huu uanze mara moja,” amesema.


Mapema, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile ambaye pia ni Mbunge wa Mufindi Kusini alimwomba Waziri Mkuu atoe neno ili kujibu kilio cha muda mrefu cha wanaMufindi ambacho ni ujenzi wa barabara Nyololo hadi Mtwango yenye urefu wa km. 40 na ile ya Mafinga hadi Mgololo yenye urefu wa km.80.


“Barabara hizi ni kiungo muhimu sana kwa uchumi wa Mufindi. Huku tuna viwanda vingi, tuna mashamba makubwa ya chai kwa hiyo tunahitaji barabara imara ili tuweze kusafirisha mazao kwenda sokoni na kuleta malighafi za viwanda vyetu,” alisema.


Aliishukuru serikali kwa kupeleka huduma za umeme, elimu kwenye jimbo hilo.

Post a Comment

0 Comments

Close Menu