Blog Post

VIPAUMBELE NANE KUHARAKISHA MAPINDUZI YA KIDIJITALI MHE KAIRUKI

Na Omary Mbaraka 


Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imetangaza vipaumbele nane vya utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2026/2027, ikiwa ni mkakati wa kuimarisha sekta ya mawasiliano, kupanua huduma za kidijitali na kukuza uchumi wa kidijitali nchini.


Akiwasilisha bajeti ya Wizara hiyo bungeni leo 30 Aprili, 2026 Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki(Mb) ameomba kwa niaba ya Wizara hiyo kuidhinishiwa jumla ya shilingi 222,589,451,000 kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27 ambapo Serikali inalenga kuharakisha maendeleo ya miundombinu ya TEHAMA ili kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi wote, hususan walioko maeneo ya vijijini.


Waziri Kairuki alitaja vipaumbele nane vikiwemo ujenzi na uimarishaji wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, hatua itakayoongeza kasi, usalama na ubora wa huduma za intaneti. 


Vilevile, Serikali itaendelea kuboresha mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi ili kurahisisha utoaji wa huduma za kijamii, kiuchumi na kiserikali.


Aidha, Wizara imeweka mkazo katika kuongeza upatikanaji wa mawasiliano vijijini ili kuhakikisha wananchi wa maeneo ya pembezoni hawabaki nyuma katika mapinduzi ya kidijitali, Sambamba na hilo, Serikali itaendelea kuimarisha uwezo wa taasisi za umma katika utekelezaji wa majukumu ya TEHAMA ili kuongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji.


Katika kukuza ubunifu na ajira, Wizara imepanga kuendeleza ujenzi wa vituo vya ubunifu vya TEHAMA (ICT Parks) vitakavyosaidia kukuza vipaji vya vijana na kuibua suluhisho za kiteknolojia. Hatua hii inalenga kuchochea ubunifu na kuongeza mchango wa vijana katika maendeleo ya uchumi wa kidijitali.


Vipaumbele vingine ni pamoja na kuimarisha huduma za serikali mtandao (e-Government), kuongeza usalama wa mtandao (cyber security), kukuza ujuzi wa TEHAMA kwa vijana na kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi. Kwa ujumla, vipaumbele hivi vinalenga dhamira ya Serikali ya kujenga Tanzania ya kidijitali yenye mawasiliano imara, jumuishi na bunifu kwa manufaa ya wananchi wote.


#BajetiyaMawasiliano2026/27.

Post a Comment

0 Comments

Close Menu