Na Omary Mbaraka 

Mkuu wa Mkoa wa Manyara nchini Tanzania Queen Cuthbert Sendiga amewataka Wanawake wakiwemo Viongozi kufahamu nafasi zao kwenye ndoa pindi wakiwa majumbani kwa kuwa Mwanamke kufahamu haki yake haimaanishi aache kumuheshimu Mumewe na kuota masharubu akisema

Wanaume wanahitaji pia kutunzwa.


RC Queen amesema hayo wakati akiongea na Jumuiya ya Wanawake wa CCM Mkoani humo ikiwa ni mwendelezo ya maadhimisho ya miaka 49 tangu kuzaliwa kwa CCM ambapo amesema hadi sasa Mkoa wa Manyara una kesi zaidi ya 80 za vitendo vya

ukatili wa kijinsia.


"Wakina Mama amkeni na kufahamu nafasi zenu na thamani zenu, Mwanamke kufahamu haki yako hakumaanishi usimuheshimu Mumeo, hiyo ndio changamoto nyingine wakina Baba wanajua akina Mama wakijitambua ndani ni moto, tukisimama hapa sisi ni Viongozi tukirudi ndani sisi ni Wake na akina Mama wa Familia lazima tujue kucheza na nafasi hizo mbili,” Queen amesema.


Amesema muda mwingine wanapata matatio kwa sababu ya wao kujifanya wana masharubu ndani huku akiweka wazi kuwa ndani ya nyumba mwenye sharubu ni mmoja tu ambaye ni Mwanaume hivyo wanawake wanapodai haki zao wanapaswa pia kutimiza haki zao nyumbani kama akina Mama.


“Mama tangu asubuhi kiguu na wewe miguu inanukia kama mbuzi anayechomwa, akina Baba nao wana mioyo wanataka kutunzwa, wewe muda wa kutunza Mume hauna, muda wa kutunza Watoto hauna tukusaidie vipi?, Mama una vikoba nane huna sehemu ya kupata pesa unamtia Mumeo sukari bure tendo la ndoa ndani hawezi unakwenda kwa Vijana wa Bodaboda, ukija hapa pepeta nyumbani kuwa zuzu ndivyo mahaba yanavyotaka mahaba haitaki kelele,” Queen ameendelea kusema.


Aidha amewataka akina Mama kuamka na kufahamu nafasi zao pamoja na thamani zao huku akisema Mwanamke kufahamu haki yake hakumaanishi asimuheshimu Mume wake na hiyo ndio changamoto nyingine wakina Baba wanajua akina Mama wakijitambua ndani ya nyumba ni moto.


“Tukisimama hapa sisi ni Viongozi tukirudi ndani sisi ni Wake na akina Mama wa Familia lazima tujue kucheza na nafasi hizo mbili,” Queen amemaliza kwa kusema hayo.