Na Mdoe Kiligo
MKUU wa Mkoa wa Mwanza Mhe.CPA. Amos Makalla ametangaza mkakati kamambe wa kutatua kero za wananchi Mkoani humo kwa kuwashirikisha Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na Makatibu Tawala wa Wilaya.
Akizungumza kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa katika kikao kazi na viongozi hao, Mhe. Makalla amesema atafanya uzinduzi huo Septemba 18 mwaka huu na kuwaagiza Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Makatibu Tawala wa Wilaya wahudhurie ili wapate mwongozo mzuri watakapokwenda kushughulika na kero za wananchi.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema utaratibu huo ameufanya kwenye mikoa yote aliyofanya kazi hivyo anaamini utaratibu huo kwa Mkoani Mwanza utakuwa na tija kwa Serikali kuwa karibu zaidi na wananchi.
"Nawaagiza viongozi wenzangu mara baada ya uzinduzi huo wa kusikiliza kero za wananchi, muende sehemu zenu za kazi na kuweka mpango kazi wa kuwatembelea wananchi kila kata na baadaye ziwasilishwe kwenye Halmashauri kwa kufanyiwa kazi", amesisitiza CPA Makalla.
Amesema manufaa ya kusikiliza kero hizo zinawapunguzia mzigo wananchi yakiwemo mashauri yaliyopo mahakamani yanayohusu migogoro ya ardhi na mengineyo na kusisitiza utaribu huo usiishie kusikiliza tu bali pia kutoa majibu, kushauri na mwelekeo wa jambo husika.
Amewaagiza pia watumishi wa Idara za ardhi kwenye Halmashauri waweke utaratibu wa kuwahudumia wananchi hasa migogoro ya ardhi na mipaka.
"Nimeunda kikosi kazi maalum ambacho kitapita kwenye Halmashauri zote kupata taarifa za migogoro ya ardhi niwaombe viongozi wote mtoe ushirikiano kwa kiosi kazi hiki", CPA Makalla.
Ameongeza kuwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi waunde timu ya pamoja na kuitangaza bayana miradi yote ya maendeleo kwa wananchi na kusikiliza changamoto na muendelezo wa miradi hiyo na shule zote na hospitali ziwe na mipaka ili kuepuka kuingiliwa.
0 Comments