Na Mdoe Kiligo
KATIKA kuweka mikakati ya kujiimarisha kiutendaji na kuendeleza ushirikiano wa kimataifa, Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) Septemba 7 mwaka huu 2023 limekutana na ujumbe kutoka Chuo cha Huanggang Polytechnic (HPC) cha nchini China, uliokuja Tanzania kujielimisha kuhusu mazingira ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa lengo la kukuza ushirikiano katika nyanja hiyo kupitia fungamano la China-Afrika kwenye masuala ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.
Ugeni huo ukiongozwa na Mkuu wa Chuo cha HPC, Bw. Jiang Anxin, umejadiliana na NACTVET kuhusu masuala ya viwango vya kazi na namna chuo hicho kinavyoweza kuanzisha kituo cha umahiri wa kazi za ufundi hapa nchini.
Aidha, ukiwa nchini, ujumbe huo utatembelea idara za elimu kufahamu hali ya jumla ya elimu ya ufundi, mahitaji ya kiufundi ya soko nchini, elimu ya ushirika, masuala ya viwango, mafunzo ya ujuzi, mpango wa kubadilishana wanafunzi wa kimataifa na masuala ya tamaduni kati ya China na wenyeji, Tanzania.
Wakati wa ukaribisho, Katibu Mtendaji wa NACTVET, Dk. Adolf Rutayuga amesisitiza kwamba Baraza kama chombo rekebu cha masuala yote ya TVET nchini, lipo tayari kutoa msaada utakaohitajika kwa chuo cha HPC kuanzisha kituo cha kukuza ujuzi hapa nchini, na hata kuunganisha mashirikiano baina ya HPC na vyuo vya TVET vya Tanzania ambavyo vimesajiliwa na kuidhinishwa na NACTVET kutoa mafunzo ya ufundi.
Kikao hicho kimehudhuriwa pia na wakurugenzi na wakuu wa vitengo mbalimbali wa NACTVET.
Wakati huohuo, Dkt. Rutayuga amewataka “Risk Champions” wa Baraza, kuwa jicho la kuyabaini mapungufu yanayoweza kuathiri utendaji wa taasisi na kushauri ipasavyo ili kuleta tija mahali pa kazi. Dkt. Rutayuga amewaaasa washiriki wakati wa zoezi la kupitia Risk Management Register ya NACTVET Septemba 9 Septemba 2023, mjini Morogoro.
Dkt. Rutayuga amekumbusha umuhimu wa wakurugenzi na wakuu wa vitengo ndani ya Baraza kupitia Risk Register mara kwa mara ili kuweza kutimiza malengo ya Taasisi kiujumla.
Amewapongeza na kuwahimiza Risk Champions wa kila Idara na Kitengo kutumia fursa hiyo kuainisha maeneo yanayoweza kuathiri utendaji kazi wa Baraza ili yaboreshwe, pia ameagiza Semina hii itolewe kwa wafanyakazi wote.
Mafunzo hayo yamewezeshwa na Mkaguzi mwandamizi kutoka wizara ya fedha, idara ya makaguzi mkuu wa serikali Bw. Felix Kapesula
0 Comments