Blog Post

HATUTOKUWA NA HURUMA KWA WANAOWAONEA WANYONGE - KIKWETE

Na Omar Mbaraka

NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora  ambaye pia ni Mbunge wa Chalinze mkoani Pwani, Ridhiwani Kikwete ameanza ziara ya Mkoa wa Mara kwa kutembelea na kuongea na Watumishi wa Manispaa ya Musoma na kisha kufanya ziara kukagua utekelezaji wa mpango wa kuondoa Umaskini yaani TASAF katika Mji huo. 

Naibu Waziri ambaye ana ziara ya siku tatu katika Mkoa huo aliwaelekeza Watumishi wa Umma kujikita katika kuhakikisha wanazingatia na kutafsiri maono ya Rais Samia Suluhu Hassan pale aliwahimiza kuwe na Utumishi wenye kuleta tija, ubora wa  kimkakati unaolenga kuwatumikia wateja ambao ni wananchi. Akizungumza na watumishi,  Naibu Waziri aliwaasa kuwa wabunifu na wenye mikakati ili kufikia malengo.

Pia katika tukio jingine Ndg. Kikwete amewaondoa kwenye Uratibu wa mpango wa TASAF Waratibu wa Mkoa na wale wa Wilaya kwa kile alichokiita kushindwa kufikia malengo ya kuwahudumia wananchi wanyonge ambao wanahitaji sana huduma hiyo katika muda muafaka.

 Akionyesha kukasirishwa na kushindwa kwao  Mhe. Kikwete alimueleza Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Ndugu Msalika Robert  Makungu kutoelewa kwa nini hadi leo wahitaji hao hawajalipwa wakati Fedha kwa ajili ya wanufaika zilishatumwa kwa ajili ya wanufaika hao. 

Naibu Waziri anaendelea na ziara Mkoani hapo kwa kuelekea Wilayani Tarime. 




Post a Comment

0 Comments

Close Menu