Na, WAF- New York
Tanzania imetoa wito kwa nchi za Afrika na wadau mbalimbali wa sekta ya kuweka mikakati endelevu ili kuharakisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria.
Akizungumza katika mkutano wa ngazi ya juu uliofanyika New York leo kuhusu kuimarisha ubunifu wa ndani na kuharakisha matumizi ya zana mpya za kukabiliana na malaria,Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amesema nchi za Afrika zinapaswa kuchukua jukumu kubwa zaidi katika kuendeleza, kugharamia na kuhakikisha upatikanaji wa zana zinazohitajika kuondokana na malaria.
Alisema umuhimu wa jambo hilo ni mkubwa, akieleza kuwa malaria inaendelea kusababisha vifo vya mamia ya maelfu ya watu kila mwaka, huku Afrika ikibeba sehemu kubwa zaidi ya mzigo huo.
“Ni vigumu kupata familia Tanzania ambayo haijawahi kukesha usiku mzima na mtoto akiwa na homa, wakitumaini kuwa ni homa ya kawaida tu. Mara nyingi huwa ni malaria,” Mchengerwa alisema.
Alisisitiza kuwa mapambano dhidi ya malaria hayawezi tena kutegemea pekee teknolojia zinazoagizwa kutoka nje au ufadhili wa kimataifa, akisema nchi za Afrika zinahitaji kujenga uwezo wa kuzalisha bidhaa muhimu za afya karibu na jamii zinazozihitaji.
Kwa mujibu wa Mchengerwa, Tanzania tayari imejijengea historia katika kuchangia ubunifu na maendeleo ya teknolojia za kukabiliana na malaria.
Alieleza kuwa Tanzania ilianza mapema kuzalisha vyandarua vyenye dawa za kuua mbu jijini Arusha, huku Kibaha kukiwa na uzalishaji wa viuatilifu vya kibiolojia vinavyolenga kuua mazalia ya mbu kabla ya mbu hao kukua na kuwa mbu kamili.
Tanzania pia imekuwa ikishiriki katika tafiti za kutathmini teknolojia mpya za kuzuia malaria. Mchengerwa alitaja utafiti mkubwa uliofanyika Misungwi, Mkoa wa Mwanza, ambao ulisaidia kutoa ushahidi kuhusu ufanisi wa vyandarua vyenye viambata viwili vya kuua mbu.
Waziri huyo alisema uzoefu huo unaonyesha kuwa nchi za Afrika hazipaswi kuwa watumiaji pekee wa ubunifu unaozalishwa katika maeneo mengine duniani, bali zinapaswa kuendelea kuwa vituo ambako teknolojia mpya zinafanyiwa utafiti, majaribio, uzalishaji na hatimaye kutumika.




0 Comments