Blog Post

SERIKALI KUPITIA UPYA MFUMO WA BIASHARA NA UCHIMBAJI WA MADINI YA TANZANITE


 Na Mwandishi wetu 

Rais Samia Apongezwa Kwa Kuelekeza Asilimia 10 ya mapato ya Sekta ya Madini kwenye utafiti wa kina wa madini

Waziri Mavunde aelekeza nguvu ya Utafiti madini wa kina Mirerani

Atoa wiki 2 kwa wazalishaji wakubwa kuja na mpango wa kuongeza uzalishaji

Kofia Ngumu Zenye Kamera Maalum Kuanza Kutumika Kufuatilia Uchimbaji Chini ya Migodi

Wizara za Madini na Wizara ya Nishati Zaja na Mkakati wa Umeme Maeneo ya Shughuli za Madini

Serikali Yafungua Njia ya Mitaji Kupitia Dhamana za Mikopo

Mirerani, Manyara.

Serikali kupitia Wizara ya Madini imeanza kuchukua hatua za kuboresha mfumo wa biashara na uchimbaji wa madini ya Tanzanite nchini, kwa kufikia maamuzi yaliyotokana na taarifa za Tume na Kamati zilizoundwa kuchunguza changamoto za sekta hiyo, kwa ajili ya kuboresha mazingira ya biashara, kuimarisha usimamizi na kuongeza uzalishaji wa madini hayo adimu duniani sambamba na kuongeza thamani.


Mhe. Mavunde ametoa maelekezo hayo, Agosti 24, 2026, wakati wa ziara ya kukagua shughuli za uchimbaji na biashara ya Tanzanite Mirerani, Wilaya ya Simanjiro, ambapo ametembelea migodi inayomilikiwa na Franone Mining & Gems Co. Ltd. Na Chusa Mining Limited,soko dogo la madini,eneo la uthaminishaji na jengo la biashara ya madini ya Tanzanite.

Aidha Waziri Mavunde, ametoa wiki mbili kwa wachimbaji wa kati wa madini ya Tanzanite Mirerani kuwasilisha taarifa ya hatua wanazochukua katika kutumia teknolojia za kisasa za utafiti, akisisitiza kuwa sayansi na teknolojia ni muhimu katika kubaini mashapo yaliyopo na kuongeza uzalishaji wa madini hayo adimu duniani sambamba na kuacha uchimbaji wa kubahatisha kwa kukosa taarifa sahihi.

"Wekezeni kwenye teknolojia ya kisasa ya utafiti, wekezeni kwenye sayansi ili kubaini mashapo yaliyopo. Ndani ya wiki mbili kuanzia nataka kupata taarifa ya juhudi zenu za uwekezaji katika teknolojia ya kisasa ya utafiti,” amesema Mhe. Mavunde.

Aidha, Waziri Mavunde amempongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maelekezo ya kutenga asilimia 10 ya mapato yatokanayo na Sekta ya Madini kwa ajili ya utafiti, akisema uamuzi huo utaongeza kasi ya utafiti wa kina wa rasilimali za madini nchini.

Amesema Mirerani na Mkoa wa Manyara ni miongoni mwa maeneo ya kipaumbele katika mpango huo wa utafiti, hatua inayolenga kuongeza uelewa wa rasilimali zilizopo na kuwezesha shughuli za uchimbaji kufanyika kwa ufanisi zaidi.

Akizungumzia upatikanaji wa mitaji, Mhe. Mavunde amesema wachimbaji wanaweza kunufaika na mikopo nafuu kupitia taasisi za fedha, huku Serikali ikiendelea kuimarisha mifumo ya dhamana za mikopo.

Amesema Shirika la Mfuko wa Dhamana za Mikopo (Credit Guarantee Scheme Corporation) kupitia Benki Kuu ya Tanzania tayari umeundwa na kusajiliwa, na unatarajiwa kusaidia wachimbaji kupata mitaji kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao.

Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde, ametangaza kuanza kutumika kwa kofia ngumu yenye kamera katika migodi ya Mirerani, teknolojia itakayowezesha ufuatiliaji wa shughuli za uchimbaji hata chini ya mgodi kwa kuanza na Mgodi wa Franone Mining & Gems Co. Ltd na kuelekeza migodi mingine kutumia teknolojia hiyo ili kuongeza ufanisi katika usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za uchimbaji.

Kuhusu changamoto ya nishati ya umeme, Mhe. Mavunde amesema Wizara ya Madini na Wizara ya Nishati zimeweka mkakati wa pamoja wa kuhakikisha upatikanaji wa nishati unaendana na mahitaji ya Sekta ya Madini, ili shughuli za uchimbaji na shughuli zingine zinazoambatana na Sekta ya Madini ziendelee bila vikwazo.

Post a Comment

0 Comments

Close Menu