Na Mwandishi wetu
Wafanyabiashara na abiria wanaotumia Kituo cha Mabasi cha Makumbusho, Manispaa ya Kinondoni, wameiomba Serikali pamoja na mamlaka husika za mazingira kuingilia kati hali ya uchafuzi wa mazingira unaotokana na mlundikano wa taka katika kituo hicho, wakihofia kuzuka kwa magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu na magonjwa mengine ya tumbo.
Wakizungumza na Tafakari News Weblog wafanyabiashara hao walisema taka zimekuwa zikizagaa kwa muda mrefu karibu na maeneo ya kuuzia vyakula, jambo linaloweka afya za wananchi katika hatari kubwa.
Mfanyabiashara wa vyakula katika eneo hilo, Ali Hamisi Mwita, alisema hali ya usafi katika kituo hicho imeendelea kuzorota huku mkandarasi anayehusika na ukusanyaji wa taka akionekana kutotekeleza wajibu wake kwa wakati.
"Tunaiomba Serikali ifike haraka kunusuru hali hii. Taka zimejaa karibu na maeneo ya biashara za vyakula, jambo ambalo ni hatari kwa afya za wananchi, hasa wanawake na watoto. Hatujui kama gari la mkandarasi limeharibika au kuna tatizo gani, lakini hali imekuwa mbaya sana," alisema Ali.
Kwa upande wake, Maria Daudi, ambaye pia ni mfanyabiashara katika eneo hilo, alisema zimepita takribani wiki mbili bila taka kuondolewa.
"Ni muda wa wiki mbili sasa hakuna zoezi la kuzoa taka. Harufu mbaya imeongezeka na mazingira haya yanaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko. Tunaomba mamlaka husika zichukue hatua za haraka kabla hali haijawa mbaya zaidi," alisema Maria.
Baadhi ya abiria waliokutwa kituoni hapo walieleza wasiwasi wao kuhusu mazingira ya kituo hicho, wakisema kuwa uchafu uliopo karibu na maeneo ya chakula unaweza kuhatarisha afya za watu wengi wanaopita na kutumia huduma katika kituo hicho kila siku.
Jitihada za chombo hiki cha habari kuzungumza na Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ili kupata ufafanuzi kuhusu sababu za kuchelewa kuondolewa kwa taka hizo hazikufanikiwa, baada ya kutopatikana hadi wakati wa kuchapisha habari hii.
Wananchi wamezitaka mamlaka husika kuchukua hatua za haraka za kusafisha eneo hilo na kuhakikisha huduma ya ukusanyaji taka inafanyika kwa wakati ili kuzuia athari za kiafya zinazoweza kujitokeza.







0 Comments