Na Omary Mbaraka
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Namibia, Dkt. Nandi-Ndaitwah ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi wamekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili ili kufungua fursa zaidi za maendeleo kwa wananchi wa pande zote.
Akizungumza leo Juni 20, 2026 jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesema katika mazungumzo yao ya ana kwa ana wameweka mkazo katika kuongeza ushirikiano katika sekta mbalimbali za kiuchumi zenye uwezo wa kuleta matokeo chanya kwa pande zote.
Amesema Serikali ya Tanzania inawataka wafanyabiashara wake kuchangamkia fursa zilizopo nchini Namibia, huku pia akiwakaribisha wafanyabiashara wa Namibia kuwekeza na kufanya biashara nchini Tanzania.
Rais Samia amebainisha kuwa maeneo ya ushirikiano huo ni pamoja na usalama wa chakula, uchumi wa buluu, biashara, pamoja na sekta ya mafuta na gesi, ambazo zote zina nafasi kubwa ya kuchochea ukuaji wa uchumi.
Ameongeza kuwa ushirikiano huo unalenga kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na kiuchumi, huku ukichochea ubadilishanaji wa uzoefu na teknolojia kati ya nchi hizo mbili.
*RAIS DKT. SAMIA: NAMIBIA KUIMARISHA MATUMIZI YA KISWAHILI*
Kutokana na lugha ya Kiswahili kukua kwa kasi kimataifa, majadiliano kati ya Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Netumbo Nandi-Ndaitwah wa Namibia yamegusia namna ya kuongeza matumizi ya lugha hiyo nchini humo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema tayari Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Chuo cha Triumphant College cha Namibia vimeanza ushirikiano wa kufundisha Lugha ya Kiswahili.
Aidha, Serikali ya Tanzania imeunga mkono hatua hiyo na kukubali ombi la Serikali ya Namibia la kuwafundisha Kiswahili watendaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo.
Rais Samia ameeleza hayo, Juni 20, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya mazungumzo yake na Rais Nandi-Ndaitwah wa Namibia.



0 Comments