Blog Post

KAULI YA UDASA DAR ES SALAAM


 Na Mwandishi wetu

Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA), imepasua mbarika na kuilipua Serikali kwa hoja nzito, ikidai kuwa machafuko ya Oktoba 2025 ni zao la "ndoa haramu" kati ya wizi wa mali za umma na vitendo vya kikatili vya utekaji nyara wa raia.


Kupitia tamko la kishujaa la "Jicho la UDASA," wasomi hao wamechambua kero 53 zinazofukuta nchini, wakisisitiza kuwa amani ya Tanzania imeingia doa si kwa bahati mbaya, bali kwa makusudi ya viongozi waliolewa madaraka, walioacha kulinda raia na kuanza kujitajirisha huku wakitumia vyombo vya dola kukandamiza wanaodai haki kwa kutumia nguvu na vitisho.


Wasomi hao wameinyooshea kidole Serikali kwa kile walichokiita "uongo wa waziwazi" na kiburi cha watumishi wa umma ambao wamegeuka miungu watu, wakijilimbikizia mali kupitia ubadhirifu huku vijana (Gen-Z) wakizama kwenye dimbwi la umaskini, ukosefu wa ajira, na msongo wa mawazo uliokithiri.


UDASA imebainisha kuwa wizi wa rasilimali za taifa umesababisha kufeli kwa huduma muhimu za kijamii, jambo lililozalisha hasira ya kijamii ambayo Oktoba 2025 iligeuka kuwa volcano iliyolipuka baada ya wananchi kuona kura zao hazina thamani mbele ya "wezi wa demokrasia" na mifumo ya uchaguzi iliyopoteza uhuru na uhalali mbele ya macho ya umma.


Katika hali ya kustaajabisha, tamko hilo limeweka bayana kuwa vitendo vya watu kutekwa na kupotezwa vimekuwa ni sumu inayotafuna uzalendo, huku Jeshi la Polisi likituhumiwa kugeuka kuwa chombo cha kutisha raia badala ya kuwalinda kama sheria inavyoelekeza.


UDASA imeeleza kuwa ukosefu wa haki katika Mahakama na ukimya wa kutisha wa Idara ya Usalama wa Taifa dhidi ya madhila ya wananchi, kumejenga picha ya taifa linaloendeshwa kwa mabavu, ambapo mwananchi anayehoji wizi wa viongozi anajibiwa kwa vitisho, utekaji, au nguvu ya silaha, hali iliyofuta kabisa dhana ya kihistoria ya Tanzania kama "kisiwa cha amani."


Mwenyekiti wa UDASA, Dkt. Elgidius Ichumbaki, ametoa onyo kali kuwa uponyaji wa kitaifa hautapatikana kwa hotuba za kuliwaza bali kwa Serikali "kujishusha, kukiri makosa, na kuleta Katiba Mpya" itakayowawajibisha wezi na watekaji waliojificha ndani ya mamlaka.

Post a Comment

0 Comments

Close Menu