Blog Post

BALOZI WA MAZINGIRA AHAMASISHA WANANCHI KUPANDA MITI WAKATI WA MVUA

 Na Omary Mbaraka 

Balozi wa mazingira wa kujitolea, Moses Mwakibolwa, amewataka wananchi kote nchini kutumia fursa ya mvua zinazoendelea kunyesha kupanda miti ili kuimarisha ikolojia na kupunguza athari za uharibifu wa mazingira ikiwemo upepo mkali unaosababisha madhara mbalimbali.

Akizungumza kuhusu maandalizi ya uzinduzi wa mkakati wa Darasa la Mazingira, utakaofanyika tarehe 04 Aprili 2026 katika eneo la Boko CCM, Kata ya Bunju, Manispaa ya Kinondoni, Mwakibolwa amesema Watanzania wanapaswa kujenga utamaduni wa kupanda miti kila mara kunapokuwa na unyevunyevu wa kutosha ardhini ili kuongeza kasi ya upandaji miti nchini.

Amesema miti ya kupanda inapatikana kwa wingi katika bustani za Tanzania Forest Services Agency (TFS), na kinachohitajika kwa wananchi ni kutenga muda na kujitolea kupanda miti katika maeneo wanayoishi.

Kwa upande wake Mwakibolwa ameitaka Tanzania Electric Supply Company Limited (TANESCO) kuacha kukata miti katika maeneo ya wananchi bila kushirikisha serikali za mitaa.

Amesema miti inayopandwa na wananchi mara nyingi hugharimu fedha na nguvu nyingi, hivyo ni vyema TANESCO wakashirikiana na wananchi kwa kutoa ushauri wa maeneo sahihi ya kupanda miti badala ya kusubiri miti ikue na baadaye kuikata bila mpango.

Aidha, amesisitiza kuwa TANESCO pia inaweza kushiriki kikamilifu katika kampeni ya kitaifa ya upandaji miti ili kulinda mazingira na kusaidia juhudi za serikali na wananchi katika uhifadhi wa mazingira

Post a Comment

0 Comments

Close Menu