Na Mwandishi wetu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anaendelea kuthibitisha uimara wa diplomasia ya Tanzania katika jukwaa la kimataifa baada ya kumpokea Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China, Mheshimiwa Wang Yi, aliyefanya ziara ya kikazi nchini Tanzania. Mapokezi na mazungumzo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, yanaakisi uongozi thabiti wa Rais Samia katika kuimarisha mahusiano ya kimataifa yanayolinda maslahi ya Taifa.
Katika mazungumzo hayo, Mheshimiwa Wang Yi aliwasilisha salamu za dhati kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mheshimiwa Xi Jinping, jambo linalodhihirisha heshima na hadhi kubwa ambayo Tanzania inaendelea kupata kimataifa chini ya uongozi wa Rais Samia.
Uhusiano wa Tanzania na China una historia ndefu ya kindugu ulioanza rasmi mwaka 1964, na umejengwa juu ya misingi ya kuheshimiana, usawa na kutoingiliana katika masuala ya ndani, huku miradi ya kihistoria kama reli ya TAZARA ikibaki kuwa alama ya mshikamano wa kweli kati ya mataifa haya mawili.
Ziara hii ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China inaendelea kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya Tanzania na China, kufungua fursa mpya za maendeleo na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika diplomasia ya kikanda na kimataifa.
Kwa ujumla, mapokezi haya ni uthibitisho wa mafanikio ya diplomasia ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuiweka Tanzania kama taifa lenye heshima, ushawishi na mwelekeo thabiti wa kimataifa.




0 Comments