Na Mwandishi wetu
Rais wa Venezuela aliyetekwa nyara na Marekani, Nicolas Maduro ameiambia mahakama jijini New York kwamba "hana hatia", "ni mtu staarabu", na kwamba alikuwa "ametekwa nyara", katika matamshi yake ya kwanza hadharani tangu kujiri shambulio la kuogofya la Marekani dhidi ya nchi yake Jumamosi.
Maduro, ambaye alitekwa nyara pamoja na mkewe na vikosi maalum vya Marekani kutoka nyumbani kwake huko Caracas katika operesheni iliyolaaniwa sana kote duniani kwa kuwa ilikanyaga sheria ya kimataifa, alifikishwa katika mahakama ya shirikisho jana Jumatatu kwa ajili ya kusikilizwa kwa kesi inayodaiwa kuwa "ugaidi wa mihadarati" na mashtaka mengine.
Maduro na mkewe, Cilia Flores, walifikishwa mbele ya Jaji wa Marekani, Alvin K Hellerstein saa 12 jioni Jumatatu kwa kesi fupi inayofugua ukurasa wa mvutano mrefu wa kisheria kuhusu iwapo wanaweza kukabiliwa na kesi nchini Marekani au la.
Maduro alikanusha mashitaka dhidi yake, akimwambia jaji kuwa, "Nilitekwa nyara. Mimi sina hatia na ni mtu mstaraabu, (mimi ningali) rais wa nchi yangu."
Haya yanajiri huku maelfu kwa maelfu ya Wavenezuela wakiendelea kumiminika katika barabara na mitaa ya Caracas, kushiriki maandamano makubwa ya kulaani uchokozi wa Marekani kufuatia kutekwa nyara kwa Rais Maduro.
Wakati huo huo, Bunge la Venezuela limemuidhinisha Delcy Rodríguez kuwa rais wa mpito wa nchi hiyo, siku mbili baada ya vikosi vya Marekani kumteka nyara Maduro. Rodriguez alikula kiapo cha uongozi wakati wa sherehe fupi iliyofanyika katika Bunge la Kitaifa jana Jumatatu, akiwaambia wabunge kwamba alikuwa akifanya hivyo "kwa jina la Wavenezuela wote."



0 Comments