Na Omary Mbaraka 


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ambaye pia ni Mbunge wa Kundi la Vijana kupitia Chama Cha Mapinduzi (Viti Maalumu - CCM), Ng’wasi Kamani, amesema ataendelea kulisemea, kulitetea na kulipambania kundi la vijana kupata fursa mbalimbali za kujiinua kiuchumi, hususan katika sekta ya mifugo na uvuvi.


Ng’wasi ameyasema hayo, Desemba 24, 2025, wilayani Iramba, mkoani Singida, alipomwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi, Dkt. Mwigulu Nchemba, katika kikao cha Baraza la Kawaida la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani humo.


“Pamoja na majukumu haya niliyopewa, sitachoka kumtetea, kumsemea na kumpambania kijana wa Kitanzania. Hata katika sekta hii ninayoisimamia nitapandisha jitihada ili, ikiwezekana, sekta zingine pia ziige mfano wa kumsaidia kijana wa Kitanzania,” amesema Ng’wasi.


Aidha, Ng’wasi amesema yuko tayari kushirikiana na vijana katika kufikia fursa za kiuchumi na kuwahimiza vijana, kuwa mstari wa mbele katika kukemea vitendo vya uvunjifu wa amani nchini, pamoja na kumwombea mema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.