Blog Post

TAASISI YA GST YATOA USHAURI NA UPIMAJI SAMPULI ZA MAJI, MIAMBA NA MADINI

 Na Omary Mbaraka 


Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imeendelea kutoa ushauri na huduma za upimaji wa sampuli za miamba na madini kwa wananchi mbalimbali wanaofika kutaka kujua aina za miamba na madini  waliokuwanayo.


Aidha, GST imekuja na vifaa vya utafiti wa miamba na madini iliyo chini ya tabaka ya juu la udongo ambavyo kitaalam vinaitwa vifaa vya  jiofizikia.


Sambamba na hayo, Wataalamu kutoka GST wamewashauri wananchi kutumia Maabara ya taasisi hiyo kwa uchunguzi wa sampuli zao za  miamba na madini ili kubaini wingi na uwepo wa madini ili kuongeza tija na uzalishaji wa madini.


Aidha, Wizara ya Madini kwa kushirikiana na taasisi zake imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya sekta ya madini kupitia banda lake lililopo katika eneo la mabanda ya Serikali, banda namba 5.


Kupitia banda hilo, wananchi wanaelimishwa kuhusu shughuli mbalimbali zinazohusu sekta ya madini zikiwemo Utafiti wa Madini, Sheria na Kanuni zinazosimamia sekta hiyo, Taratibu za kisheria za kuendesha shughuli za madini, biashara ya madini pamoja na mbinu bora na salama za uchimbaji wa madini.


Lengo kuu la utoaji wa elimu hiyo ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata uelewa sahihi kuhusu namna ya kushiriki kikamilifu katika sekta ya madini kwa kuzingatia Sheria na Miongozo iliyopo, huku wakihimizwa kufanya shughuli hizo kwa njia endelevu, salama na zenye tija.


Pamoja na mambo mengine, Wizara inawaalika wananchi wote kutembelea banda hilo ili kujifunza zaidi kuhusu fursa mbalimbali zinazopatikana katika sekta ya madini, na namna ya kuzitumia kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.


Wizara ya Madini itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha elimu hii inawafikia wananchi wengi zaidi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha na kuendeleza sekta ya madini nchini.

Post a Comment

0 Comments

Close Menu