Blog Post

ARDHI NDIYO ITAKAYOMWINUA RAIS SAMIA AMA KUMDIDIMIZA

 Na Omary Mbaraka 

Rais wa kwanza Mwalimu Julius Kambarage Nyerere enzi za uhai wake akiwa madarakani alitoa falsafa yake ya maendeleo akisema katika nchi yetu, ili tuendelee tunahitaji haya manne;

(i) Watu

(ii) Ardhi

(iii) Siasa safi na

(iv) Uongozi bora.

Kwanini Nyerere alianza na watu? Kwasababu hata hii dunia yetu iliumbwa ili ikaliwe na watu. 

Kwahiyo kilicho muhimu kwa maendeleo ya nchi yoyote kwanza ni hao watu wanaoimiliki nchi, kwakuwa watu ndio wanaobuni mipango ya maendeleo. Watu wanabuni mifumo ya utawala pia ndio wanaotekeleza mipango yote inayohusu maendeleo ya nchi yao.

 Lakini hao watu wanabebwa na Ardhi, kwakuwa wanaishi juu ya Ardhi, wanafanya shughuli zao zote nzuri na mbaya wakiwa juu ya Ardhi. Watu wanaitegemea Ardhi kwa yote yanayogusa maisha yao ya hapa duniani.

Katika Tanzania utajiri wa kwanza ni Ardhi, serikali ya awamu ya kwanza iliunda wizara ya Ardhi, Maliasili na Utalii, baadaye wizara ya Ardhi, nyumba na maendeleo. Ardhi ndiyo inayoubeba utajiri mwingine wote wa nchi hii, kuanzia utajiri ulio juu yake hadi ulio ndani yake, kwa maana ya madini na chemichemi za maji.

Kimsingi Ardhi ndiyo mama wa maendeleo ya binaadamu, kuanzia mtu binafsi hadi nchi ama Taifa. Hakuna Taifa linaloweza kujiendeleza wala kuwaletea wananchi wake usitawi pasipo usimamizi mzuri wa Ardhi yake.

Ndiyo maana hata Wakomunisti enzi walipokuwa wakitamba na mfumo wao wa Ukomunisti, waliweka bayana kwenye mafundisho yao, wakiitaja Ardhi kama kitivo kikuu yaani “center of materialism.” 

Kwaajili hiyo nasema katika Tanzania yetu Ardhi ndiyo inapaswa kuongoza kwa ubora, kwa maana ya kwamba wizara iwe na viongozi bora, kuanzia Waziri, Katibu Mkuu hadi watendaji walio ngazi za chini, wote wanapaswa kuwa waadilifu.

 Taasisi zote za wizara ya Ardhi zinapaswa kuwa na viongozi wakuu walio waadilifu, ili kupitia uadilifu wao waweze kusimamia vyema utendaji ama operesheni zote zinazohusu Ardhi yetu ili ziende katika uadilifu. 

Hapo ndipo Tanzania itapata maendeleo kwani bila uadilifu kwenye wizara yetu ya Ardhi maendeleo ya Mtanzania yatarudishwa nyuma tu, kwasababu hali ya kukosekana uadilifu kwenye rasilimali kuu ya Ardhi, kutazalisha mabaya mengi kama rushwa, uzembe na ufisadi. Hayo yakitawala kwenye Ardhi yetu lazima yataturudisha nyuma kwakuwa yatagusa maisha yetu ya siku kwa siku.

Hadi sasa wizara ya Ardhi ndiyo inayoongoza kwa wingi wa migogoro, kesi na mashauri yanayohusu Mtanzania kugongana na Mtazania mwingine kwa namna moja ama nyingine. Huko vijijini kuna migogoro mingi inayohusu Ardhi, wakulima na wafugaji kugombea maeneo kwasababu hakuna maeneo rasmi yaliyotengwa kwaajili ya wafugaji kuchunga mbali na wakulima.

Kuna migogoro mingi ya wakulima kugombea mipaka wao kwa wao kwasababu tu mashamba yao hayajapimwa wala wakulima kupewa hati miliki ili waweze kuitumia Ardhi yao kibiashara. 

Kuna kesi nyingi zinazohusu watu kudaiwa kuvamia maeneo ya wengine, ama serikali za vijiji kudaiwa kuvamia maeneo ya watu binafsi. 

Kwenye miji na Halmashauri za miji kuna tatizo la watumishi wa Ardhi kukosa uadilifu katika kugawa viwanja, wapo wataalamu wanaotengeneza hati za bandia na kusababisha raia wema kuaminishwa kwamba wamepokea hata halali kumbe hati hizo zikiwa siyo halali.

Wapo watendaji kwa kukosa uadilifu wametoa hati miliki zilizo halali lakini zimetolewa kwa watu zaidi ya mmoja, yanapotokea mambo ya aina hii uhalisia wake ni kwamba raia wema ndio wanaogombanishwa na kulazimishwa kuipambania haki yao Mahakamani. 

Kutokana na ukweli kwamba mashauri yaliyo Mahakamani hayatakiwi kuingiliwa na nguvu nyingine kutoka nje ya Mahakama, basi hizo mahakama zinapochelewa kutoa uamuzi wa mwisho huwa zimezuia kiwanja ama eneo husika kuendelezwa. Kiuhalisia hilo linakwamisha maendeleo ya nchi.

 Kwasababu kiwanja kilichostahili kuendelezwa aidha kwa kujengwa nyumba ya kuishi ama kujengwa jengo la biashara, kinapokuwa hakiendelezwi kwasababu shauri lake liko kwenye Mahakama ambayo hailazimishwi wala haishinikizwi, uhalisi wake ni kwamba maendeleo ya nchi nzima huwa yanasimamishwa.

Kwakuwa serikali pale ilipostahili kukusanya kodi kutoka kwa watu aidha wanaouziana viwanja ama wanaomiliki, hukosa kodi zote kutokana na viwanja hivyo kuwa kwenye migogoro. Serikali hukosa kodi ya majengo ambayo ingekusanywa kutoka kwa wamiliki wa majengo na biashara ambazo zingefanyika kwenye majengo hayo kwasababu tu maeneo yaliyopaswa kuendelezwa huwa hajaendelezwa. Hii maana yake ni Mtanzania kukosa kufaidika na utajiri asilia wa Ardhi.

Ardhi ndiyo inabeba hata utajiri wetu wa misitu, wanyama pori, madini hadi maji ya maziwa makubwa, mito mikubwa na chemichemi zote zinazobubujika maji. Kwahiyo nchi inatakiwa iwe na sera nzuri ya Ardhi pia iwe na watendaji wazuri kwenye maeneo yote yanayogusa Ardhi, kwani sera nzuri peke yake haitoshi kwani sera inahitaji utekelezaji.

Nchi ikiwa na Ardhi nzuri lakini sera za Ardhi zikiwa mbaya, huo uzuri wa Ardhi na rutuba yake havitawanufaisha wananchi! Nchi ikiwa na sera nzuri ya Ardhi lakini wizara ya Ardhi ikawa na watendaji wabaya ama Taasisi na vitengo vyake vikawa na viongozi wabovu, huo uzuri wa sera hautawanufaisha wananchi.

Ndio maana nasema Ardhi ndiyo itakayomwinua “boost” Samia ama kumdidimiza! Kwasababu Ardhi inamhusu kila mtu, kwa sasa Watanzania wengi wamajeruhiwa mioyoni mwao, wengi wanalia kutokana na walivyoumizwa na mambo ya hovyo yanayoendeshwa kwenye wizara yetu ya Ardhi na vitengo vyake na Taasisi zake.

Wengine mashauri yao yanahitaji kutatuliwa ndani ya dakika moja tu, mhusika kusema ndiyo au hapana ili hatua zingine zichukuliwe. Lakini bado yamekwamishwa kwa miezi ama miaka, kimsingi hawa ndio wapinga maendeleo wa kwanza katika nchi yetu.

Pia Kuna baadhi ya wanasheria ambao si waadilifu hupenda migogoro ya ardhi kuendelea ili wao wapate fedha hivyo maafisa ardhi wanapaswa pia kuwa MAKINI na wanasheria wa namna hio.

Post a Comment

0 Comments

Close Menu