Blog Post

LEO XIV PAPA MPYA WA KANISA KATOLIKI DUNIANI


Na Omary Mbaraka 

Kardinali Robert Prevost ametangazwa kuwa kiongozi ajaye wa Kanisa Katoliki. Yeye ndiye Papa wa kwanza kutoka Marekani na kuchukua jina la Papa Leo XIV.

Kanisa Katoliki limempata kiongozi wake mpya, Papa Leo wa 14 atakayewaongoza takriban waumini bilioni 1.4 kote ulimwenguni. 

Kiongozi huyo amepatikana Alhamisi jioni baada ya uchaguzi uliofanywa na makadinali wapatao 133 kutoka mataifa 70.

Papa Leo XIV, ambaye jina lake la kuzaliwa ni Robert Francis Prevost, alizaliwa huko Chicago Septemba 14, 1955. 

Prevost alisoma katika Umoja wa Kitheolojia wa Kikatoliki wa Chicago, akitunukiwa diploma ya theolojia.

Akiwa na umri wa miaka 27, alikwenda Roma kusomea sheria za kanuni katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Thomas Aquinas (Angelicum). 

Mafunzo yake ya kidini yalimfikisha Peru kama mmishionari, na baadaye akafanikiwa kupata nyadhifa mbalimbali nchini Marekani na Peru.

Prevost aliongoza dayosisi ya Chiclayo huko Peru na alikuwa makamu wa pili wa rais wa mkutano wa maaskofu wa Peru.  Papa Francis alifahamiana naye katika nchi hiyo ya Amerika Kusini na mwaka 2023 akamteua kuwa mkuu wa Baraza la Maaskofu, na kumfanya kuwa kardinali.

Baraza la Maaskofu ni idara ya wahudumu wa  Kanisa Katoliki. Katika jukumu hilo, amehusika na uteuzi wa maaskofu duniani kote kwa miaka miwili iliyopita. Wakati huo huo, Prevost alikuwa rais wa Tume ya Kipapa ya Amerika ya Kusini.

Mwaka 2003 Papa Leo wa 14 aliwahi kutembelea Tanzania mikoa ya Dar es salaam, Songea na Morogoro ambapo alilala Morogoro kwa siku tatu. Pia alipokuwa akirudi kutoka Songea kwenda Morogoro akiwa njiani aliomba kuendesha gari na kukubaliwa.


Post a Comment

0 Comments

Close Menu