Na Ismail Mang'ola, Dar
Ujenzi wa jengo la ghorofa linalojengwa katika mazingira hatarishi eneo la Kimara Stopover, jijini Dar es Salaam, limeanza kuzua taharuki kwa majirani.
Chanzo chetu Cha habari kimebainisha kuwa, jengo hilo linajengwa katika mazingira ambayo sio rafiki na majirani hao wakiamini linaweza kuja kuhatarisha maisha ya wakazi hao.
Majirani hao walisema kuwa, hofu yao ni kwamba mmiliki wa jengo Hilo hajahamisha umeme ambao umeunganishwa kwenye nyumba zao huku waya zake zikiwa zimegusa ukuta wa jengo linalojengwa kitu ambacho linaweza kuleta maafa kwa mafundi wenyewe na hata watu wengine.
Chanzo hicho kiliendelea kusema kwamba, mbali na hatari hiyo ya umeme, pia ujenzi wa jengo Hilo haujafuata taratibu za kuweka uzio ambao utazuia kuondoka kwa vitu hatarishi kama vile vipande vya matofali kuanguka, udongo, vipandevya mbao pamoja na vitu vingine vyenye kuhatarisha usalama wa wakazi hasa watoto.
TafakarinewsWeblog baada ya kupata taarifa hizo kutoka kwenye vyanzo vyake kilifika kwenye eneo la tukio na kujionea hali halisi ambapo waandishi wa Tafakari walifanikiwa kuzungumza na mmiliki wa jengo Hilo aliyejitambulisha kwa jina la Happy ambapo alikiri kuwepo mapungufu hayo.
"ni kweli Kabisa nakiri kuwepo kwa mapungufu haya, lakini sidhani kama hili suala litakuwa la mmiliki, maana Mkandarasi alishalipwa chake, na jukumu la uondoshaji umeme alipaswa yeye ashughulikie". Happy alisema.
Majengo ya aina hii yamekuwa yakijengwa mitaani Kama njugu huku mengine yakiwa hayana vibali vya ukandarasi kwa maana ya kutosajili miradi katika Bodi ya ukandarasi CRB na ERB Hali inayoonesha ni ukwepaji wa Kodi za Serikali.
Kutokana na uchunguzi unaoendelea kufanywa na chombo hiki, toleo lijalo, tutawaletea majibu kutoka vyombo husika vya ujenzi ambavyo ni CRB, ERB pamoja na jina kamili la mmiliki wa jengo.
0 Comments