Na Steven Mhando
Dar es Salaam. Mbunge wa Kigamboni (CCM), DK Faustine Ndugulile amefariki dunia usiku wa leo Jumatano, Novemba 27, 2024 nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu.
Taarifa ya kifo hicho imetolewa na Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson. Amesema taarifa zaidi kuhusu msiba huo itatolewa.
Dk Ndugulile Alikuwa Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Dunia Kanda ya Afrika (WHO) ambaye alipaswa kuanza majukumu hayo mapya Februari 20
'Dkt Tulia Ackson alisema 'Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani, Kanda ya Afrika, Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile. Kwa niaba ya Wabunge ninatoa pole kwa familia, wakazi wa Kigamboni na Watanzania wote.'' Alisema Spika Tulia.
Naye Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa salamu za pole kwa familia, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wananchi wa Kigamboni, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote.
Dkt Ndugulile pia alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Afya ya Bunge la Tanzania, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Mabunge ya Kimataifa (IPU) Advisory Group Health na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Mtandao wa Kamati za Afya za Bunge la Afrika (NEAPACOH).
Dk. Ndugulile aliwahi kuwa naibu waziri wa Afya wa Tanzania kati ya 2017-2020, pia aliwahi kuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari 2020-2021.
Pia alifanya kazi kama mkurugenzi katika Wizara ya Afya Tanzania anayeshughulikia huduma za uchunguzi na pia meneja wa programu mwanzilishi wa Huduma ya Kitaifa ya Usambazaji Damu mwaka 2006.
Kati ya 2007-2010, aliwahi kuwa Mshauri Mkazi wa Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) nchini Afrika Kusini akitoa msaada wa kiufundi kwa nchi nyingine nyingi kama vile Angola, Msumbiji, Tanzania na Rwanda.
0 Comments