Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
JAMII imeonywa kuwa makini na matumizi ya nyanya zilizosagwa maarufu kama "tomato sauce" ambazo huzalishwa na baadhi ya Viwanda hapa nchini.
Ushauri huo umetolewa na mmoja wa madaktari hapa nchini Hussein Maulid ambaye amesema kumekuwa na wingi wa tomato sauce hizo ambazo zimesambazwa kwa wingi mitaani hasa visiwani Zanzibar zikiwa hazina viwango na hazijathibitishwa na Mamlaka husika.
Daktari huyo Bingwa wa Chakula na Lishe amesema tomato sauce hizo zimaweza kuwa na madhara makubwa kiafya, ikiwemo walaji kupata saratani.
Kiafya, amesema tomato sauce hizo zinaweza kuwa mbaya zaidi na amezitaka Mamlaka husika kuchukua hatua za haraka kudhibiti bidhaa hizo ambazo kwa Zanzibar imekuwa kama Jalala.
"Bahati mbaya Zanzibar imekuwa kama Jalala la bidhaa mbovu. Watu wanajifungia ndani na kuzalisha bidhaa zao kisha wanazimwaga mitaani, watu wanakula bila kujali viwango", amesema.
" Nimesikia kuna Viwanda feki vinavyozalisha tomato katika maeneo haya ya Unguja na hata Pemba. Kibaya zaidi bidhaa hizo zipo madukani na watu wananunua, wanatumia. Licha ya kuhatarisha afya za walaji, lakini pia watu hawa wanahujumu Viwanda halali ambavyo bidhaa zao zimethibitishwa, na wanalipa Kodi", amesema.
Lakini pia amewataka Waandishi wa Habari kuongoza kampeni ya kufichua bidhaa hizo, akisema huo ndiyo wajibu wao mkubwa kwa nchi.
"Waandishi mtatishwa sana, lakini msiogope. Isaidieni nchi katika kufichua mambo yenye madhara kwa jamii. Uzalendo kwa nchi unaanzia katika kusaidia umma wa wengi", amesema.
Moja ya habari ambazo ziliripotiwa hivi karibuni na mojawapo ya chombo kimoja cha habari ni kuenea kwa bidhaa hizo za nyanya katika maduka mbalimbali zikiwa hazina usajili wa Mamlaka ya Chakula Zanzibar.
0 Comments