Na Mwandishi wetu, dodoma
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya
imeendelea kujiimarisha katika utayari wa kukabiliana na Matukio ya dharura ya
afya ya jamii, magonjwa ya mlipuko na Matukio yenye athari za afya ya
jamii kwa kutoa mafunzo elekezi kwa Waratibu wa Mikoa wa vituo vya uratibu
Matukio ya dharura za afya ya jamii (PHEOC)
Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Grace
Magembe wakati akifungua mafunzo ya Waratibu wa Mikoa wa vituo vya uratibu
Matukio ya dharura za afya ya jamii, pamoja na Waratibu wa ufuatiliaji wa
magonjwa na Matukio yenye athari za afya ya jamii.
Amesema lengo la serikali ni kuhakikisha watanzania wanakuwa salama na afya
bora ili kufanya shughuli zao za kiuchumi na kujenga taifa kwa ujumla.
Aidha Dkt. Magembe amesema kujengewa uwezo kwa wataalam hao kutasaidia
kuharakisha uchakataji wa taarifa na kuchukua hatua madhubuti na za haraka za
udhibiti wa matukio hayo.
Ameeleza kuwa mikoa hiyo 11 ni mikoa ya awali ya kipaumbele kutokana na
uwezekano wa kupata dharura mbalimbali kama magonjwa ya mlipuko kutokana na
jiografia na mwingiliano wa kiuchumi katika Mikoa hiyo.
“Mikoa na Halmashauri ni ngazi muhimu katika kuleta mabadiliko (game changer)
kwenye udhibiti wa matukio ya dharura ya afya ya jamii ikiwemo magonjwa ya
milipuko”. Amesema Dkt. Magembe.
Kwa kuongezea amesema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mikakati ya kukabiliana na
magonjwa ya dharura ikiwemo magonjwa ya mlipuko na ajali mbalimbali.
Mafunzo hayo yamejumuisha waratibu kutoka mikoa 11 kutoka Tanzania bara na
visiwani chini ya ufadhili wa Kituo cha kukinga na kudhibiti Magonjwa cha
Afrika (Africa CDC), Marekani (US CDC) na Shirika la Afya Duniani.
Dkt. Magembe amesema kuwa mafunzo hayo ni sehemu mikakati iliyowekwa na
serikali ili kuhakikisha wanailinda nchi na majanga, maafa ikiwemo magojwa ya
mlipuko na ajali.
Pia Dkt. Grace amesema hivi karibuni Tanzania ilifanyiwa tathmini na Dunia
kuona utayari wa kukabiliana na dharura za magonjwa ya mlipuko, maafa na
majanga.
“Kwa tathmini iliyofanyika mwaka 2006 Tanzania ilikuwa na asilimia 48 na kwa
sasa matokeo ya awali tuna asilimia 63 za utayari wa kukabiliana na dharura za
magonjwa ya mlipuko, maafa na majanga”. Ameeleza Dkt. Magembe.
0 Comments