Na Mwandishi Wetu Marekani
MGOMBEA wa Chama cha Democratic, Scott Colom, ameshinda kinyang'anyiro cha kuwania nafasi ya useneta katika Jimbo la Mississippi nchini Marekani, akiipa chama hicho ushindi wa kushtua katika jimbo linalotawaliwa kwa kiasi kikubwa na misimamo ya kihafidhina na ambalo kwa miongo kadhaa limekuwa likichagua wagombea wa Chama cha Republican.
Ni Mwekezaji wa Tanzania pia
Ushindi huo umemfanya Colom kuwa mtu wa kwanza mweusi kutoka Mississippi kuingia katika Seneti ya Marekani tangu Blanche Bruce, aliyehudumu katika nafasi hiyo kuanzia mwaka 1875 hadi 1881.
Colom ametenganishwa na mpinzani wake wa Republican, Cindy Hyde-Smith, ambaye alikuwa seneta aliyekuwa madarakani, kwa kura zisizozidi 5,000 kati ya takribani kura milioni moja zilizohesabiwa.
Matokeo hayo yana maana kuwa chama cha Democratic kitakuwa na viti 55 kati ya 100 vya Seneti, huku matokeo ya kinyang'anyiro kingine katika Jimbo la Alaska yakiwa bado hayajatangazwa rasmi.
Hyde-Smith alitumia mtandao wa kijamii wa X Jumatano jioni kuweka video ya kumpongeza Colom kwa ushindi huo na kumtakia kila la heri katika majukumu yake mapya.
"Ingawa matokeo haya si yale tuliyoyafanyia kazi wala tuliyokuwa tukiyatarajia, ninaheshimu uamuzi wa wapiga kura wa Mississippi," alisema.
Ushindani huo haukuonekana kuwa na ushindani mkubwa hadi katika wiki za mwisho za kampeni, kutokana na Rais Donald Trump kushinda jimbo hilo katika uchaguzi wa mwaka 2024 kwa tofauti ya zaidi ya asilimia 22.
Colom alitoa hotuba yake ya ushindi katika Chuo cha Tougaloo, ambako alipokelewa na mamia ya wafuasi waliokuwa wakishangilia huku wakiwa wamesimama bega kwa bega chini ya anga la usiku.
Kulikuwa na shamrashamra wakati alipowashukuru wafuasi wake kwa kumuunga mkono katika kipindi chote cha kusubiri matokeo tangu uchaguzi uliofanyika Novemba 4.
Wakati huo huo, mamia ya watu walikusanyika katika makao makuu ya Chama cha Kitaifa cha Kutetea Maendeleo ya Watu Weusi (NAACP) yaliyopo Jackson, Mississippi, Jumatano, wakati ushindi wa Colom ulipotangazwa.
Tangazo hilo lilipokelewa kwa shangwe na makofi makubwa kutoka kwa watu waliokuwa ndani ya ukumbi huo.
Mwenyekiti wa Bodi ya NAACP, Leon Russell, alisema ushindi huo ni matokeo ya kipekee.
"Haya ni matokeo ya kushangaza," alisema Russell.
Aliongeza kuwa ushindi huo umetokana kwa kiasi kikubwa na juhudi za jamii ya watu weusi.
"Haya ni matokeo ya kazi kubwa iliyofanywa hasa na jamii ya watu weusi. Hakukuwa na fedha nyingi, lakini kulikuwa na juhudi kubwa za kujipanga na kuhamasishana," alisema.
Alisisitiza kuwa uchaguzi huo utaendelea kukumbukwa kama tukio la kihistoria.
Katika ukumbi huo, ambako watu walikuwa wakikumbatiana kwa furaha, mmoja wa wafuasi hao, Amber Thomas, alisema ushindi huo umeleta furaha kubwa kwake.
Katika kampeni zake, Colom alifanya jitihada za kuwafikia hata wapiga kura wa Chama cha Republican. Aliwahi kwenda katika mkutano wa kampeni za Trump na kuzungumza na watu waliokuwa kwenye foleni nje ya eneo la mkutano huo.
Tukio jingine lililompa umaarufu ni pale mpinzani wake, Hyde-Smith, alipoulizwa kuhusu kupanda kwa bei ya nyama ya ng'ombe na kumshauri mpiga kura kuchagua aina nyingine ya protini.
Colom alilitumia jibu hilo katika tangazo lake la kampeni lililosambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii.
Hyde-Smith, ambaye amekuwa akihudumu katika Seneti tangu mwaka 2018, alionekana kushindwa kuhimili wimbi la kutoridhishwa kwa wananchi dhidi ya Chama cha Republican katika ngazi ya taifa.
Kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa baada ya wapiga kura kupiga kura, hasira za wananchi dhidi ya chama cha Trump zilitokana kwa kiasi kikubwa na changamoto za kiuchumi, ambazo zilihusishwa na sera za ushuru wa bidhaa zinazoingizwa nchini Marekani pamoja na vita dhidi ya Iran.
Colom, ambaye ni mwendesha mashtaka katika eneo lake, alitumia hali hiyo kujijengea uungwaji mkono kwa kuikosoa sera ya ushuru wa bidhaa ya Trump na kuonyesha namna mpinzani wake alivyounga mkono sera hizo.
Katika kampeni zake, alimpa Hyde-Smith jina la utani la "Cindy High Prices", akimaanisha Cindy wa bei za juu, akitumia suala la gharama za maisha kama moja ya ajenda kuu za kumshambulia kisiasa.
Aidha, Colom alifanya kampeni kubwa kwa kutembelea kaunti zote 82 za Jimbo la Mississippi ili kuwafikia wapiga kura katika maeneo mbalimbali.
Kwa upande wake, kampeni za Hyde-Smith zilimshambulia Colom kwa kumtaja kuwa kibaraka wa mfadhili tajiri wa siasa za mrengo wa kiliberali, George Soros, ambaye familia yake imesaidia kuchangia fedha katika kampeni za kisiasa za mgombea huyo wa Democratic.
Mkurugenzi mkuu pamoja na uongozi wa chombo hiki cha Tafakari unatoa pongezi nyingi kwa bw Scott Colom kwa ushindi hasa tukizingatia kuwa ni mmoja wa wawekezaji hapa Tanzania katika mahoteli ya kisasa Moja ipo katika mbuga za wanyama Sadani ijulikanayo Cyttera Sadani Hotel na nyingine iliopo morogoro mjini ijulikanayo Nashera Hotel




0 Comments