Blog Post

KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA NA TAASISI ZAKE

 Na Mwandishi wetu 


KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeipongeza Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na taasisi zake, ikiwemo Tume ya Ushindani (FCC) na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kwa hatua zinazochukuliwa katika kutekeleza majukumu yao na kuboresha mazingira ya biashara nchini.


Pongezi hizo zimetolewa leo Agosti 19, 2026 na  Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Deodatus Mwanyika,  wakati wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa shughuli za Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia taasisi zake, kilichofanyika Bungeni jijini Dodoma.


Mwanyika amesema juhudi zinazofanywa na Wizara pamoja na Taasisi zake zimeanza kuonyesha matokeo chanya, hususan katika kuimarisha mazingira ya biashara, uzalishaji na uwekezaji nchini.


Amesema pamoja na mafanikio hayo, Serikali inapaswa kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya bidhaa bandia na hafifu zinazoingia sokoni, kwa kuwa bidhaa hizo zinaweza kusababisha hasara kwa wazalishaji wa ndani na kuhatarisha afya pamoja na usalama wa watumiaji.


Aidha ameitaka Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na taasisi zake kuendelea kuimarisha mifumo ya udhibiti na ukaguzi wa bidhaa, huku hatua stahiki za kisheria zikichukuliwa dhidi ya watu wanaojihusisha na uzalishaji, uingizaji na uuzaji wa bidhaa zisizokidhi viwango.


Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), amesema Wizara imepokea maelekezo na ushauri uliotolewa na Kamati hiyo na kwamba itaufanyia kazi kwa lengo la kuboresha huduma na kuongeza ufanisi katika sekta ya viwanda na biashara.


Kapinga amesema Wizara itaendelea kushirikiana na taasisi zilizo chini yake kuhakikisha maelekezo yanayolenga kuimarisha mazingira ya biashara na kulinda maslahi ya wazalishaji na watumiaji yanatekelezwa kwa ufanisi.


Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), Bi. Khadija Ngasongwa, amesema taasisi hiyo inaendelea kutekeleza wajibu wake wa kusimamia ushindani wa haki katika soko na kuchukua hatua dhidi ya wanaokiuka sheria na masharti ya biashara.


Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Godfrey Nyaisa, amesema taasisi hiyo inaendelea kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watu na wafanyabiashara wanaokiuka masharti yaliyowekwa, huku ikiendelea kuboresha huduma zake kwa wafanyabiashara nchini.


Kwa ujumla, kikao hicho kimeendelea kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Bunge, Wizara na Taasisi zake katika kuhakikisha sekta ya viwanda na biashara inakuwa na mazingira wezeshi, yenye ushindani wa haki na yanayolinda maslahi ya wazalishaji pamoja na watumiaji.




Post a Comment

0 Comments

Close Menu