Na Mwandishi wetu
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb), amepokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Jamhuri ya Shirikisho la Nigeria nchini, Mhe. Rahmat Mohammed Omobolanle, katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika tukio hilo, Waziri Kombo amemkaribisha Balozi Mteule Rahmat nchini, amemtakia utekelezaji mwema wa majukumu yake ya kidiplomasia, amemuhakikishia Balozi Rahmat ushirikiano wa muda wote atakapokuwa nchini na kueleza umuhimu wa kuendelea kuimarisha uhusiano wa kihistoria na wa kindugu uliopo kati ya Tanzania na Nigeria.
Viongozi hao pia wamejadili masuala mbalimbali yenye maslahi ya pamoja, hususan namna ya kuimarisha zaidi ushirikiano wa kiuchumi kupitia maeneo ya biashara, uwekezaji, elimu, usafirishaji, burudani na sanaa pamoja na maeneo mengine ya maendeleo.
Naye Balozi Mteule Rahmat Mohammed Omobolanle akizungumza baada ya kuwasilisha Nakala za Hati zake za Utambulisho alipongeza namna uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano kati ya Nigeria na Tanzania ulivyo na kuongeza kuwa atahakikisha uhusiano huo unazidi kuimarika na kufika mbali zaidi.
Alimuhakikishia Mheshimiwa Waziri Kombo utayari wake wa kufanya kazi kwa karibu na serikali ya Tanzania kwa lengo la kukuza na kuimarisha zaidi uhusiano uliopo na hivyo kutekeleza kwa vitendo Sera ya Mambo ya Nje ya Nigeria.







0 Comments