Na Omary Mbaraka
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amezindua rasmi Soko Kuu la Kariakoo lililokuwa katika ukarabati tangu mwaka 2022, kufuatia ajali ya moto iliyoteketeza mali zote zilizokuwemo ndani ya soko hilo.
Ufunguzi huo umefanyika leo Februari 8, 2026, katika eneo la soko hilo jijini Dar es Salaam, ambapo wafanyabiashara na wananchi pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali na vyama vya siasa wamehudhuria.
Baada ya ajali hiyo, Serikali ilitoa Sh28 bilioni kwa ajili ya ukarabati wa soko hilo. Kati ya fedha hizo, sehemu ilitumika kujenga soko dogo jipya lenye ghorofa sita.
Ukarabati wa soko kuu umehusisha ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya kudhibiti majanga ya moto, miundombinu rafiki kwa watu wenye mahitaji maalumu pamoja na uwekaji wa lifti kwa ajili ya kubeba watu na mizigo, hali inayolifanya Soko la Kariakoo kuwa la kisasa zaidi.
*RAIS DKT. SAMIA: UGAWAJI WA MAENEO SOKO LA KARIAKOO UFUATE HAKI*
Rais Samia Suluhu Hassan amesema kukamilika kwa Soko Kuu jipya la Kariakoo lililopo mkoani Dar es Salaam kunaleta mageuzi makubwa ya kibiashara, baada ya maboresho yanayowawezesha wafanyabiashara wengi kupata nafasi ya kufanya biashara zao kwa utaratibu mzuri na wenye tija.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa soko hilo leo Februari 8, 2026, akiwa mgeni rasmi, Rais Samia amesema anahitaji kusikia usawa bila upendeleo na ukiritimba wakati wa ugawaji wa maeneo ya biashara, hususan kwa wale waliokuwepo awali na kuathirika na ajali ya moto.
Rais Samia ameongeza kuwa haitakuwa busara kwa viongozi wa Serikali Mkoa wa Dar es Salaam na wenye mamlaka katika soko hilo kujipa kipaumbele kwenye fursa za kugawa maeneo ya biashara, na kuwataka wasimamie kwa haki, hasa kwa wafanyabiashara waliolengwa kufanya biashara ndani ya soko hilo.
Aidha, Rais Samia amesisitiza kuwa mamlaka za mapato zisimamie ukusanyaji wa kodi kwa weledi, huku akisisitiza uwazi katika taarifa za mapato na matumizi ya fedha za soko hilo la kimataifa.
Soko jipya la Kariakoo limejengewa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 28, likiboresha miundombinu na kutoa nafasi kubwa zaidi kwa wafanyabiashara kufanya biashara ndani ya soko.
Ujenzi huo umefanywa kufuatia moto ulioharibu soko la awali, ili kurejesha shughuli za biashara na kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara kwa wafanyabiashara waliokuwa wakilitumia soko la zamani.
*RAIS DKT. SAMIA AAGIZA MATUMIZI MIFUMO YA KIELEKTRONIKI KUKUSANYA KODI SOKO KUU KARIAKOO*
Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza umuhimu wa kutumia mifumo ya kidijitali kusajili wafanyabiashara wote wanaofanya biashara ndani ya Soko Kuu la Kariakoo ili kuongeza uwazi katika ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha kila mfanyabiashara analipa kodi stahiki.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Februari 8, 2026 wakati akizindua Soko Kuu la Kariakoo jijini Dar es Salaam, ambapo ameeleza kuwa kuwepo kwa kanzidata ya wafanyabiashara kutasaidia mamlaka husika kufahamu mahali alipo kila mfanyabiashara, aina ya biashara anayofanya pamoja na kiwango cha kodi anachotakiwa kulipa.
Amesema matumizi ya mifumo ya kielektroniki yataondoa mianya ya ukwepaji kodi na kurahisisha ufuatiliaji wa mapato ya masoko, huku akisisitiza kuwa uwazi wa mapato na matumizi ni jambo muhimu katika uendeshaji wa masoko.
“Tunapokuwa na mifumo thabiti ya ukusanyaji mapato, tunaweza kumtambua kila mfanyabiashara, mahali alipo na kiwango cha kodi anachopaswa kulipa, hivyo hakuna atakayebaki bila kulipa,” amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia amesisitiza kuwa kukosekana kwa uwazi katika mapato na matumizi kunaweza kusababisha migogoro na hata vitendo vya uharibifu, akihimiza viongozi na wasimamizi wa masoko kuhakikisha taarifa za mapato na matumizi zinakuwa wazi ili kulinda rasilimali za umma na kuimarisha imani ya wafanyabiashara.
*RAIS DKT. SAMIA APIGA MARUFUKU VIGOGO KUHODHI VIZIMBA SOKO LA KARIAKOO*
Rais Samia Suluhu Hassan amepiga marufuku viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Wilaya ya Ilala kuhodhi maeneo na vizimba katika Soko Kuu la Kariakoo, kisha kuwakodisha wafanyabiashara wadogo.
Rais Samia ametoa agizo hilo leo Jumapili, Februari 8, 2026, wakati akizindua Soko Kuu la Kariakoo jijini Dar es Salaam, ambalo limefanyiwa ukarabati mkubwa na upanuzi ili kuongeza tija kwa wafanyabiashara.
Akizungumza kwa msisitizo mbele ya viongozi na mamia ya wananchi waliojitokeza katika uzinduzi huo, Rais amesema kuwa mfumo wa ukodishaji wa maeneo ndani ya soko hilo unapaswa kuwa wa wazi na kusimamiwa na Shirika la Masoko Kariakoo pekee.
"Nisingependa kusikia hapa nazungumza na wakubwa wa jiji la Dar es Salaam na Wilaya ya Ilala, nisingependa kusikia ninyi wakubwa ndio mnahodhi maeneo humu ndani na kuwakodisha watu," ameonya Rais Samia.
*RAIS DKT. SAMIA AAGIZA UREJESHWAJI WA WAFANYABIASHARA SOKO KUU LA KARIAKOO BILA UPENDELEO*
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameagiza Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) kuhakikisha mchakato wa kuwarejesha wafanyabiashara waliokuwepo awali katika Soko Kuu la Kariakoo unafanyika kwa haki, uwazi na bila upendeleo wowote.
Akizungumza leo Februari 8,2026 wakati wa uzinduzi wa soko hilo jipya, Rais Samia alisema katika soko la zamani kulikuwepo na mfumo wa upangishaji usiofuata utaratibu, hali iliyosababisha kukosekana mapato na kuzua malalamiko miongoni mwa wafanyabiashara.
Rais alikumbusha kuwa alipolitembelea soko hilo kabla ya ujenzi mpya, alikuta wafanyabiashara wengi wamebanana ndani ya soko huku wengine wakifanya biashara nje kwa kukosa vibanda, jambo lililoonyesha wazi uhitaji mkubwa wa kuwa na soko la kisasa na masoko mengine ya aina hiyo nchini.
“Tumejifunza kutokana na yaliyopita. Leo hatujarekebisha tu soko lililoungua, bali tumejenga soko jipya lenye ghorofa sita na huduma mbalimbali kwa wafanyabiashara. Ni muhimu waliokuwa ndani warudishwe bila upendeleo, na waliokuwa nje wapewe nafasi zilizopo kwa haki,” amesema Rais Samia.
Amesisitiza kuwa Tamisemi isiruhusu ukiritimba wala upendeleo katika upangaji wa vibanda, ili soko hilo liwe chanzo cha mapato kwa Serikali na mazingira bora ya kufanya biashara kwa wananchi.
*WAZIRI MKUU, DKT. MWIGULU NCHEMBA*
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Februari 08, 2026 amezindua soko jipya la Kariakoo lililopo Ilala jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba ameshiriki katika uzinduzi huo ambapo amesema kuwa uamuzi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia wa ujenzi wa soko hilo, ni ishara ya dhati ya kujitoa kwake kwa Watanzania, hususan wafanyabiashara wa Kariakoo na watumiaji wa soko hilo.
Amesema Rais Dkt. Samia ameendelea kurejesha tabasamu kwa wananchi kwa kutekeleza kwa vitendo ahadi anazozitoa, jambo linalodhihirisha uongozi wake wa vitendo na unaojali maslahi ya watu.
Ameeleza kuwa soko hilo limejengwa kwa misingi ya kisasa, kwa kuzingatia maono ya Rais Samia, ili kuhakikisha mazingira salama na rafiki kwa wafanyabiashara.
Amesema kuwa soko hilo limewekewa mifumo imara ya umeme, kamera za ulinzi pamoja na jenereta za dharura, hatua zinazolenga kuongeza usalama na ufanisi wa shughuli za biashara.
Amesisitiza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuboresha mazingira ya biashara na kukuza uchumi wa wananchi kupitia miundombinu ya kisasa na endelevu.
#KaziNaUtuTunasongaMbele
#TabasamuLaUtu
#MaendeleoEndelevu



0 Comments