Na Mwandishi wetu
Kardinali Robert Prevost amechaguliwa kuwa papa na atajulikana kama Papa Leo XIV.
Mzee huyo mwenye umri wa miaka 69 ndiye Mmarekani wa kwanza kuwa papa na ataongoza waumini wa jumuiya ya kimataifa ya Kanisa Katoliki yenye watu bilioni 1.4.
Mzaliwa wa Chicago, anaonekana kama mwanamageuzi na alifanya kazi kwa miaka mingi kama mmishonari huko Peru kabla ya kufanywa askofu mkuu huko.
Pia ana utaifa wa Peru na anakumbukwa kwa mazuri kama mtu ambaye alifanya kazi na jumuiya zilizotengwa na kusaidia kuimarisha madaraja katika Kanisa.
Kwanini Papa huchagua jina jipya?
Moja ya matendo ya kwanza ya papa mpya ni kuchagua jina jipya, kubadilisha jina la ubatizo.
Uamuzi huo ni sehemu ya mila ya muda mrefu lakini haijawahi kuwa hivyo kila wakati.
Kwa zaidi ya miaka 500, mapapa walitumia majina yao wenyewe.
Hii ilibadilika na kuwa majina ya ishara ili kurahisisha majina waliyopewa au kurejelea mapapa waliotangulia.
Kwa miaka mingi, mapapa mara nyingi wamechagua majina ya watangulizi wao wa karibu au wa mbali kwa sababu ya heshima au pongezi na kuashiria nia ya kufuata nyayo zao na kuendelea na mwenendo wa kipapa unaofaa zaidi.
Kwa mfano, Papa Francis alisema jina lake lilimtukuza Mtakatifu Francis wa Assisi, na kwamba aliongozwa na rafiki yake wa Brazil Kadinali Claudio Hummes.
Kwa nini Papa mpya amechagua jina Leo XIV ?
Papa mpya bado hajafafanua sababu ya kuchagua jina la Papa Leo XIV.
Huenda kuna sababu nyingi nyuma ya uamuzi huo, lakini jina "Leo" limetumika na mapapa wengi katika historia ya Kanisa.
Papa Leo I, anayejulikana pia kama Mtakatifu Leo Mkuu, alikuwa papa kati ya mwaka 440 hadi 461 BK.
Alikuwa papa wa 45 katika historia na alijulikana kwa kujitolea kwake kwenye masuala ya amani.
Kwa mujibu wa simulizi za kihistoria, katika mkutano kati ya Papa Leo I na Attila, mfalme wa Huni, mnamo mwaka 452 BK, inaaminika kuwa mitume Petro na Paulo walijitokeza kimiujiza, jambo lililomfanya Attila aachane na mpango wake wa kuivamia Italia.
Tukio hili lilichorwa baadaye na mchoraji mashuhuri Raphael katika mchoro wa fresco.
Leo XIII alikuwa nani?
Papa wa mwisho kuchagua jina Leo alikuwa Papa Leo XIII, Muitaliano ambaye jina lake la ubatizo lilikuwa Vincenzo Gioacchino Pecci.
Alichaguliwa mnamo 1878, alikuwa papa wa 256 kukalia kiti cha enzi cha Mtakatifu Petro na aliongoza Kanisa Katoliki hadi kifo chake mnamo 1903.
Anakumbukwa kama papa aliyejitolea kwa sera za kijamii na haki za kijamii.
Anajulikana sana kwa kutoa waraka - barua iliyotumwa kwa maaskofu wa Kanisa - iitwayo "Rerum Novarum", msemo wa Kilatini unaomaanisha "Ya Mambo Mapya".
Waraka huo ulijumuisha mada kama vile haki za wafanyakazi na haki ya kijamii.
Majina ya papa maarufu zaidi ni yapi?
Leo ni miongoni mwa baadhi ya majina maarufu ya papa.
Jina linalotumika sana ni John, aliyechaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo 523 na Mtakatifu John I, Papa na mfia imani.
Papa wa mwisho kuchagua jina hili alikuwa Mwitaliano Angelo Giuseppe Roncalli, aliyechaguliwa Papa John XXIII mwaka 1958, ambaye alitangazwa Mtakatifu na Papa Francis mwaka 2014.
0 Comments