Blog Post

KITUO CHA MIKUTANO CHA KIMATAIFA CHA MLIMA KILIMANJARO KUJENGWA ARUSHA

 






Na Mwandishi wetu, Arusha

Viongozi mbalimbali wamempogeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia na kuelekeza fedha kwa ujenzi wa kituo cha Mikutano Cha kimataifa cha Mlima wa Kilimanjaro kitakachojengwa jijini Arusha. Kituo hicho cha aina yake Afrika, jambo ambalo ni sawa na kuileta Dunia Tanzania, Kituo hicho kinajengwa kwa ubia baina ya Taasisi ya Kituo cha Mikutano Cha Kimataifa Arusha (AICC ) na Taasisi ya Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ujenzi wake utakamilika ndani ya miaka miwili.

Pongezi hizo zimetolewa Machi 8, 2025 jijini Arusha wakati wa hafla ya utiaji saini hati ya makubaliano ya Ujenzi baina ya wabia PSSSF na AICC. 

Akizungumza mbele ya waalikwa waliohudhuria Shughuli hiyo , Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Pindi Chana ambaye wizara yake ni mmoja wa mdau muhimu sana katika matumizi ya Kituo hicho, alisema wizara ya Utalii inatoa shukrani na pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Rais kwa kuelekeza  fedha za ujenzi wa kituo hicho huku akiwaomba wasimamizi kuhakikisha kuwa ujenzi unaende haraka ili uweze kutumika kwa mkutano mkubwa ukiwemo ule Mkutano wa Dunia wa masuala ya nyuki na asali  ambao unatarajiwa kufanyika nchini, 2027.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo alimshukuru Mhe. Rais kwa kutoa baraka za ujenzi wa kituo hicho utakao gharimu shilingi 385 bilioni. Pia Waziri Kombo aliishukuru taasisi ya PSSSF kwa utayari wake na kutekeleza maelekezo ya mamlaka. Akizungumzia Faida nyenginezo, Waziri Kombo alisema uwekezaji huo ni mkakati wa Serikali unaolenga kukuza utalii wa mikutano yaani conference tourism. 

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe Ridhwani J Kikwete, pamoja na kumpongeza Mhe. Rais kwa kutoa ruksa ya ujenzi wa kituo hicho, aliikumbusha hadhara kuwa ujenzi wake ni maelekezo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025 inayoelekeza umuhimu wa kujenga mazingira wezeshi na muhimu kwa ustawi wa Taifa kiuchumi, kijamii na kiutamaduni pamoja na Maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala (CCM) ya mwaka 2021. 

Naye Mwakilishi kutoka Ofisi ya Msajiri wa Hazina, Bi. Neema Musomba alisema, “Msajili wa Hazina anapongeza ushirikiano wa PSSSF na AICC, na kuwa ofisi ya Msajili wa Hazina wakati wowote itakuwa tayari kuhakikisha mradi huu unafanikiwa.”

Nao watendaji wakuu wa PSSSF na AICC kwa nyakati tofauti walisisitiza kutimiza wajibu wao ili kuhakikisha mradi huokimkakati unakamilika kama ilivyopangwa.

Post a Comment

0 Comments

Close Menu