Blog Post

Mzee Mwinyi ametuachia somo la kusameheana, kuvumiliana


Na Mdoe Kiligo

TAIFA la Tanzania limeingia tena kwenye msiba mzito. Ikiwa ni wiki mbili tu tangu tumpumzishe aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa kule Monduli mkoani Arusha, nchi inatikisika tena.

Taarifa kwamba Rais Mstaafu wa awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi ameaga dunia  ni kama kidonda kipya katika kovu la zamani. Ni kidonda kibichi, na msiba haujawahi kuzoeleka katika Jamii yoyote ile. 

Mzee Mwinyi alifariki dunia jioni ya Alhamisi Februari 29 mwaka huu katika Hospitali ya Mzena Jijini Dar es Salaam ambako alikuwa akipatiwa matibabu.

Taarifa ya kifo chake ilitangazwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye pia ametengaza siku saba ya maombolezo ya kitaifa.

Alhaji Ali Hassan Mwinyi aliyefahamika na Watanzania wengi kama Mzee Rukhsa ataendelea kukumbukwa kutokana na mapenzi yake kwa taifa hili.

Aliishi maisha ya kawaida sana, kama alivyosema Dkt Jakaya Kikwete Rais Mstaafu wa awamu ya Nne wakati wa kuaga mwili wa Mzee Mwinyi kwenye Uwanja wa Uhuru.

Huyu ni kiongozi ambaye alileta mageuzi makubwa ya kisasa na kiuchumi hapa nchini katika Uongozi wake tangu mwaka 1985 hadi 1995.

Wakati anaingia madarakani mwaka 1985 akipokea Kijiti cha Uongozi wa mkuu wa Taifa letu kutoka kwa Rais wa Kwanza Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Alhaji Mzee Mwinyi alilazimika kufanya Mageuzi makubwa ya kiuchumi ili kuifanya nchi kuwa na bidhaa zote muhimu .

Nchi ilikuwa na ukame mkubwa wa bidhaa za kawaida na Mzee Mwinyi aliruhusu kuingia kwa bidhaa kutoka nje ya nchi ili kukidhi mahitaji ya wananchi.

Sera ya soko huria ilisaidia kupatikana kwa bidhaa mbalimbali kwa bei ya kawaida kabisa, na kwa namna Moja ama nyingine Mzee Mwinyi alikomesha magendo na  ulanguzi ambao ulikuwa umeshamiri katika nchi hii. 

Ni katika mkakati huo, mageuzi makubwa yalifanywa Serikalini ambapo Mzee Mwinyi alileta sera ya Kuwajibika makazini. Kila mfanyakazi wa umma alifanya kazi kwa kiwango cha juu, na ambaye alionekana kuwa mzembe alikumbana na fagio la chuma, kwa maana ya kuondolewa katika nafasi hiyo na kupewa mtu mwingine.

Kwa wanasiasa Mzee Mwinyi kwao ndiye baba wa mageuzi makubwa ya kisiasa hapa nchini. Yeye ndiye aliridhia nchi kurejea kwenye mfumo wa kisasa wa vyama vingi.

Wakati anaruhusu kurejea kwa mfumo huo alisema kwamba kukosoana ni moja ya mambo yanayosaidia kupiga hatua kwenye maisha ya kila siku.

Lakini akasema mfumo wa vyama vingi hauna maana ya kupigana, bali kupingana kwa hoja na kuwataka Watanzania kusameheana na kuvumiliana katika nyakati zote.

"Vyama vingi visiwe chanzo cha kuleta vurugu hapa nchini. Tupingane bila kupigana, na tukosoane bila kuhitilafiana" aliwahi kusema Mzee Mwinyi wakati nchi ikiingia kwenye mfumo wa vyama vingi mwaka 1992..

Rais Mstaafu Mzee Mwinyi amefariki dunia katika Hospital ya Mzena jijini Dar Es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya Ugonjwa  wa Saratani ya Mapafu, Rais Mwinyi amefariki akiwa na Umri wa miaka  98.

Mzee Mwinyi alizaliwa Mei 8, 1925 katika Kijiji cha Kivule pembezoni mwa barabara inayotoka Dar es Salaam kwenda Kisiju Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani.

Amekuwa Rais wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kati ya mwaka 1985-1995, lakini kabla ya hapo alikuwa Rais wa  Zanzibar mwaka 1984 hadi 1985.

Amewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Misri kuanzia mwaka 1978 hadi Oktoba 1981.

Katika utumishi wake pia aliwahi kuwa Waziri wa mambo ya Ndani, na anakumbukwa kwa uamuzi wake wa kujiuzulu nafasi hiyo kutokana na mauaji ambayo yalitokea mkoani Shinyanga. 

Mzee Mwinyi ambaye amejaaliwa kupata watoto saba na wake zake Khadija na Siti Mwinyi alisomea  Ualimu Shule ya Dole Kati mwaka 1943 na 1944 Kisha kufundisha Shule ya Mangapwani mwaka 1945.

Mwaka 1954 alikwenda nchini Uingereza kusoma katika Chuo Kikuu cha Durham.

Mwaka 1961 alipelekwa na Serikali Chuo Kikuu cha Hull, Leicester nchini Uingereza.







Post a Comment

0 Comments

Close Menu