Na Mwandishi Wetu
BAADHI ya wazazi wa wanafunzi wanaosoma katika Shule ya Msingi Kirongo Juu, Samanga Wilayani Rombo wamelalamikia ukubwa wa Michango ambayo wanatakiwa kuchangia ukarabati wa Choo cha Shule hiyo ambacho kimetitia.
Wakiongea na Mwandishi wa Habari hizi wazazi hao wamesema kwamba watoto wao wametakiwa kuchangia kiasi cha shilingi 12,000 kila mmoja kwa ajili ya ukarabati wa Choo hicho cha Shule.
Mmoja wa wazazi hao amesema utaratibu wa kuchangia ni jambo jema, lakini wao mama wazazi hawajashirikishwa katika kikao chochote cha jambo hilo.
"Kuchangia sio jambo baya, lakini Mwalimu Mkuu na Kamati yake walikaa na nani na kukubaliana kiasi hicho?", amehoji.
" Sisi tulitangaziwa kwamba Kuna fedha zaidi ya bilioni 1.2 zipo kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa madarasa na vyoo. Fedha hizi zipo Halmashauri na hizo ndiyo kazi zake.", amesema.
Amesema wananchi wanalalamika kwasababu wanadhani Serikali inaweza kufanya ukarabati huo bila kuingia kwenye mifuko ya wananchi, lakini pia Michango ambayo imekuwa ikijirudia mara kwa mara inaumiza Wananchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo hakupatikana kuzungumzia jambo hilo, lakini Ofisa Elimu Msingi wa Halmashauri hiyo Alice Makule amesema kama Michango hiyo imerudhiwa na Wananchi wenyewe haina matatizo.
Hata hivyo amesema pamoja na utaratibu huo lazima Michango hiyo ipate kibali cha Mkuu wa Wilaya.
"Kama Wananchi wamekubaliana kwenye vikao sio jambo baya, maana kuna madarasa pia yamejengwa kwa nguvu ya wananchi.. Lakini pia pale ambapo vikao vimeridhia kuwa ifanyike Michango, lazima DC aridhie", amesema.
Alipoulizwa kwamba kwanini ukarabati huo usifanywe kutumia fedha za mradi wa BOOST, ambazo tayari Halmashauri ya Wilaya ya Rombo ilipewa zaidi ya shilingi bilioni 1.2 kwa kazi hiyo, Ofisa huyo amesema inawezekana Shule hiyo hapo kwenye bajeti hiyo.
0 Comments