Na Mwandishi Wetu
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeshauriwa kuzihakiki kampuni zinazotoa mikopo kwa njia mtandao.
Wananchi mbalimbali waliobahatika kuongea na Tafakari wamesema mikopo inayotolewa kupitia mitandao hiyo inakera na kuwadhalilisha.
Mmoja wa Wananchi hao Aisha Hassan Mwanjili mkazi wa Temeke Wilayani Dar es Salaam, amesema amekopa kwenye taasisi moja inayotoa mikopo kiasi cha shilingi 20,000, lakini baada ya kushindwa kurejesha kiasi cha shilingi 28,000 ambayo ni Mkopo huo na riba kwa wiki Moja, amekuwa akipigiwa simu zenye lugha ya ukakasi na wafanyakazi wa taasisi hiyo.
"Pamoja na riba kubwa wanayotoza kwa wiki, lakini mteja akichelewa kulipa kwa wakati lugha anayokutana nayo haina staha hata kidogo" amesema Aisha.
Mwananchi mwingine, Siwema Abdul amesema baada ya kupata Mkopo wa Shilingi 20,000 kutoka taasisi nyingine inayotoa mikopo hiyo alipatwa na msiba wa baba yake mzazi.
"Katika kipindi hicho kipaumbele changu ilikuwa kumsitiri baba yangu, na wahudumu wa kampuni hiyo walipopiga simu niliwaeleza kuwa nimefiwa. Mmoja akanijibu, msiba na Mkopo wetu vina uhusiano gani?. Niliumia sana kusema ukweli. Nimewalipa pesa yao baada ya msiba, lakini huku nikiwa na donge nao" amesema.
Mkurugenzi wa Utafiti wa Kituo cha Habari Dhidi ya Umasikini (MeCAP) David Mbiza amesema kwamba wanajua kwamba kumekuwa na changamoto ya ukosefu wa ustaarabu kwa wafanyakazi wa kampuni zinazotoa mikopo kupitia mitandao.
" Tumepokea malalamiko mengi, na tumefanya utafiti na kugundua kwamba kuna haja kwa Serikali kupitia upya usajili wa kampuni hizi maana haziwasaidii Wananchi bali zinawadhilisha" amesema Mbiza.
Amesema licha ya ukubwa wa riba inayotozwa na ongezeko la riba hiyo muda wa marejesho ya Mkopo ukipita, lakini utafiti wa Kituo hicho umebaini kwamba baadhi ya kampuni hizo zimeajiri wafanyakazi ambao sio wastaraabu.
" Kuna mtu mmoja ambaye alikopa na akachelewa kulipa kwa wakati, kampuni iliyotoa Mkopo ilipiga simu sio tu kwa wadhamini wa Mkopo huo waliojazwa kwenye taarifa, bali watu wengine ambao wamo kwenye orodha ya simu ya mkopaji. Hapa unajiuliza, kampuni hizi zinapata wapi sheria ya kudukua Mawasiliano ya mtu? " amehoji Mbiza.
Amesema Kituo chake kinaandaa taarifa na malalamiko ambayo yana ushahidi kwenda Benki Kuu, lakini Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuomba ufuatiliaji na hatua dhidi ya baadhi ya kampuni hizo.
0 Comments